November 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Mradi wa Uwezeshaji wa Utekelezaji wa Mwongozo wa Hiari wa kuhakikisha Uvuvi Mdogo unakuwa Endelevu (SSF) Bw. Yahya Mgawe, akifafanua namna Dawati la Jinsia katika Sekta ya Uvuvi

Dawati la jinsia sekta ya uvuvi kuimarisha usawa kijinsia

Na Edward Kondela,TimesMajira online

SERIKALI imesema uwepo wa Dawati la Jinsia katika Sekta ya Uvuvi kutasaidia kuimarisha usawa wa kijinsia pamoja na kuboresha uratibu wa serikali hususan uboreshwaji wa Sera ya Taifa ya Uvuvi juu ya mtazamo wa wanawake katika Sekta ya Uvuvi nchini.

Katibu Msaidizi wa Jukwaa la Wanawake Wanaojihusisha na Shughuli za Uvuvi nchini (TAWFA) Fatuma Katula akifafanua kuwa Dawati la Jinsia litatatua changamoto nyingi za wanawake wanaojihusiha katika sekta ya Uvuvi.

Akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt.Rashid Tamatamah, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa wizara hiyo katika Sekta ya Uvuvi Bw. Amos Machilika wakati wa uzinduzi wa dawati hilo jijini Dodoma, amesema wanawake katika Sekta ya Uvuvi wanachukua nafasi kubwa na muhimu katika mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi.

Bw. Machilika ameongeza kuwa Mwezi Novemba Mwaka 2019, serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sekta ya Uvuvi ilisaini makubaliano na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), kutekeleza Mradi wa Uwezeshaji wa Utekelezaji wa Mwongozo wa Hiari wa kuhakikisha Uvuvi Mdogo unakuwa Endelevu (SSF) katika muktadha wa uhakika wa chakula na kuondoa umasikini.

‘‘Lengo kuu la warsha hii ni kuzindua rasmi na kujenga uelewa wa pamoja juu ya Dawati la Jinsia, dawati hili lifanye kazi kwa ufanisi na kufikia malengo yote tarajiwa katika kutekelezwa kwa mpango kazi wa Dawati la Jinsia.“ Amesema Bw. Machilika

Aidha amefafanua kuwa ili kuwaunganisha na kuwatengenezea mazingira mazuri wanawake wote wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi katika Sekta ya Uvuvi nchini, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na FAO imeamua kuanzisha Dawati la Jinsia katika Sekta ya Uvuvi kwa ajili ya kutatua kero zinazowahusu wanawake na makundi yaliyo katika mazingira magumu katika Sekta ya Uvuvi na kuzipatia utatuzi.

Ametaja baadhi ya kero hizo kuwa ni kufanya kazi nzito na kulipwa ujira mdogo au kutolipwa kabisa, unyanyasaji wa kingono, ukosefu wa taarifa juu ya masoko ya bidhaa zao, ukosefu wa elimu juu ya ujasiriamali na usimamizi wa rasilimali fedha.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi Bw. Emmanuel Bulayi, Afisa Uvuvi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Abdi Hussein amesema kuwa kutokana na zoezi la utambuzi wa idadi ya vikundi vya wanawake wanaojihusisha na uvuvi wapatao takriban 6,000 wizara iliunda Jukwaa la Wanawake Wanaojihusisha na Shughuli za Uvuvi nchini (TAWFA) aidha wizara iliona ni vyema kuunda Dawati la Jinsia ili kuwafikia wanawake wote nchini na makundi maalum.

Hussein ameongeza kuwa dawati hilo litaongeza chachu katika kutatua kero mbalimbali katika Sekta ya Uvuvi hususan zinazowagusa moja kwa moja wanawake.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Mradi wa Uwezeshaji wa Utekelezaji wa Mwongozo wa Hiari wa kuhakikisha Uvuvi Mdogo unakuwa Endelevu (SSF) Bw. Yahya Mgawe amefafanua kuwa suala la usawa wa kijinsia limebainisha ushiriki wa wanawake kuwa ni mdogo katika Sekta ya Uvuvi hivyo ni muhimu kwa Dawati la Jinsia kushirikiana na wadau mbalimbali ili wanawake wawe na tija katika sekta hiyo.

Naye Katibu Msaidizi wa Jukwaa la Wanawake Wanaojihusisha na Shughuli za Uvuvi nchini (TAWFA) Bi. Fatuma Katula amebainisha kuwa baadhi ya sheria zimekuwa zikimbana mwanamke, hivyo kupitia Dawati la Jinsia changamoto nyingi zitatatuliwa na lengo ni kufika mbali na kuongeza uchumi wa nchi pamoja na nchi kuona kwamba kinapatikana chakula sahihi na bora.

Akizungumzia malengo makuu ya Dawati la Jinsia katika Sekta ya Uvuvi Afisa Uvuvi Mwandamizi Bi. Upendo Hamidu amesema litaangazia masuala yote yanayohusu wanawake zikiwemo changamoto na fursa zilizopo katika Sekta ya Uvuvi pamoja na kujumuisha makundi ya watu maalum.

Amesema dawati hilo litatumika kama kiunganishi kati ya serikali na Jukwaa la Wanawake Wanaojihusisha na Shughuli za Uvuvi nchini (TAWFA) ambapo pia dawati litaratibu masuala yote yanayohusu makundi maalum wakiwemo wanawake wenyewe, watoto na walemavu ambapo kazi kubwa ni kuhakikisha masuala ya jinsia yanajumuishwa katika Sekta ya Uvuvi ili kuleta tija kwa makundi yote maalum wakiwemo wanawake.