November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Das.Msengi:Wadau toeni ushirikiano kwa waandishi wa habari

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Wadau wa habari Kanda ya Ziwa wameombwa kuendelea kutoa ushirikiano pamoja na kuwaunga mkono waandishi wa habari ili kuleta maendeleo kwa Kanda hiyo kwa kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa uhuru na usalama.

Kwani waandishi wa habari ni kundi muhimu kwa sababu wanaelimisha jamii,kuibua masuala muhimu pamoja na kufuatilia mambo mbalimbali ya kijamii,kisiasa na kiuchumi.

Katibu Tawala Wilaya ya Ilemela Mariam Msengi akizungumza katika hafla ya usiku wa wadau wa habari na waandishi wa habari Kanda ya Ziwa,iliondaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza(MPC)

Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala Wilaya ya Ilemela Mariam Msengi akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ilemela kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,wakati wa hafla ya usiku wa wadau wa habari na waandishi wa habari Kanda ya Ziwa,iliondaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza(MPC) kwa udhamini wa taasisi na mashirika mbalimbali yenye kauli mbiu “vyombo vya habari imara ni chachu ya maendeleo ya nchi” uliofanyika Oktoba 20, mwaka huu jijini Mwanza.

“Tunaamini kwamba tasnia ya habari inapaswa kuwa uhuru na kujitegemea ,kwa umuhimu wa vyombo vya habari na msingi wa demokrasia thabiti tunapaswa kuendelea kuwaunga mkono na kuweka mazingira ambayo waandishi wa habari wanaweza kufanya kazi bila kuingiliwa na kutishiwa usalama wao,”amesema Msengi.


Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza(MPC)Edwin Soko akizungumza wakati wa Usiku wa Wadau wa Habari na Vyombo vya Habari Kanda ya Ziwa  iliondaliwa na Klabu hiyo

Kwa upande wake Mwenyekiti wa MPC Edwin Soko ameeleza kuwa lengo la hafla hiyo ni kuwakutanisha wadau wa habari na waandishi wa habari pamoja kufurahi,kujadiliana na kukosoana kwa pamoja.

Soko ameeleza kuwa wajibu wa mwandishi wa habari ni kutafuta,kuchakata na kuzitoa habari hivyo,wanaunga mkono serikali,sekta binafsi, wajasiriamali, taasisi zisizo za serikali katika kuhakikisha jamii unapata maendeleo.

“Tunajua maisha ni mafupi sana tunapokutana katika hadhira kama hii tunafurahi kwa pamoja,MPC inaendelea na jitihada za kuhakikisha waandishi wanafanya kazi katika mazingira mazuri ambapo sasa tunaendelea na mazungumzo na NHIF ili kuweza kuwaingiza katika mfuko ili wapate bima ya afya itakayosaidia kufanyakazi wakiwa salama pia wasaidiwe katika kujiendeleza kielimu ili wale ambapo hawana sifa kwa mujibu wa sheria waweze kuwa nayo,”amesema Soko.

Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis Mihayo ameeleza kuwa wamiliki wa maudhui ya mtandaoni ikiwemo radio , blogger, website na tv mtandao wanatakiwa kufuata sheria za uendeshaji wa maudhui mtandaoni.

Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis Mihayo akizungumza wakati wa Usiku wa Wadau wa Habari na Vyombo vya Habari Kanda ya Ziwa iliondaliwa na MPC

Mhandisi Mihayo pia ameutaka Muungano wa Klabu za waandishi wa Habari Tanzania(UTPC) kushughulikia Klabu za waandishi wa habari za mikoa ambazo zimekuwa na mipasuko lengo ni kujenga umoja kwa waandishi katika kufikisha huduma kwa jamii.

“Waandishi wa habari wajiendeleze kielimu kwa mujibu wa sheria,pia waanzishe blog wakiwa wamesajiliwa TCRA,UTPC hakikisheni mnaondoa tofauti zilizopo katika press club pia press club zijenge tabia ya kutembeleana ili kubadilishana uzoefu,”amesema Mhandisi Mihayo.

Naye Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Ziwa George Mhina amewapingeza waandishi wa habari kwa namna wanavyotimiza majukumu yao huku akihamasisha wananchi wawekeze katika ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini kwani masharti na vigezo vimepunguzwa ambapo ukiwa na milioni 50 utaweza kujenga kituo hicho.

Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Ziwa George Mhina