Na Heri Shaaban, Ilala
Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Charangwa Selemani, amewahimiza wahitimu wa Kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa kujitambua, kujituma na kuwa na malengo thabiti ili kutimiza ndoto zao, akisema dunia ya sasa haina nafasi kwa mtu asiyejitahidi.
Akizungumza katika mahafali ya 25 ya shule hiyo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Jokate Mwegelo, Charangwa alisisitiza umuhimu wa vijana kuwa na mipango ya maisha na kuwataka wazazi kuwalea watoto wao kwa ukaribu ili kuwaepusha na vitendo vya ukatili na mmomonyoko wa maadili.
Kwa upande wake, Mkuu wa shule hiyo, Joseph Deo, aliwapongeza wahitimu kwa nidhamu na mafanikio ya kitaaluma, huku akibainisha kuwa ufaulu wa kidato cha sita kwa mwaka 2024 umefikia asilimia 97. Aidha, alieleza mafanikio mengine ikiwemo mwanafunzi mmoja kupata nafasi ya kusoma na kucheza mpira wa kikapu Marekani, na timu ya shule kushiriki katika mashindano ya kitaifa ya michezo.
Jumla ya wanafunzi 323 walihitimu na kutunukiwa vyeti pamoja na zawadi kwa waliofanya vizuri. Walimu nao walitambuliwa kwa mchango wao katika ufaulu wa wanafunzi.
More Stories
Dkt.Jingu ahimiza matumizi ya TEHAMA katika malezi
Bil.64.5 zimetengwa kwajili ya kupanga,kupima na kumilikisha ardhi halmashauri 131 nchini
LATCU Katavi yasaidia mahitaji ya Mil.5.7 kituo cha watoto yatima,mahabusu