December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Daraja la upinde wa mawe lamaliza kilio cha wananchi

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

KUKAMILIKA kwa ujenzi wa mradi wa daraja la upinde wa mawe katika Kijiji cha Ifucha, Kata ya Ifucha katika Halmashauri ya Manispaa Tabora kumesaidia kumaliza kilio cha muda mrefu cha wakazi wa kata hiyo kupoteza mali zao katika eneo hilo kwa kusombwa na maji.

Akiongea na gazeti hili jana Naibu Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa hiyo ambaye ndiye diwani wa kata hiyo, Rose Kilimba ameeleza kuwa daraja hilo mbali na kuwa kivutio kizuri kwa wapitaji pia limeleta neema kwa wananchi.

Alisema kabla ya kujengwa daraja hilo eneo hilo lilikuwa hatarishi kwa wakazi wa kata hiyo na kata jirani ya Itonjanda kwa kushindwa kupita hasa wakati wa masika kutokana na maji kufurika hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa wanachi.

Aliongeza kuwa wakazi wengi wa kata hizo walipoteza mali zao na baadhi yao kupoteza maisha kwa kusombwa na maji hali iliyopelekea eneo hilo kuwa hatarishi na kikwazo kikubwa kwa maendeleo.

‘Tunamshukuru sana mama yetu, Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusikia kilio cha wananchi na kuwapatia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kiasi cha sh mil 149.4 ili kujengwa daraja hilo, kilio cha wananchi sasa kimeisha’, alisema.

Naibu Mstahiki Meya alifafanua kuwa kukamilika kwa daraja hilo kumerahisisha kwa kiasi kikubwa huduma za usafiri na usafirishaji bidhaa na mazao ya kilimo katika vipindi vyote vya majira ya mwaka kwa wakazi wa kata hizo.

Akielezea mradi huo Meneja wa TARURA Wilaya ya Tabora Mjini Mhandisi Manyama Tungaraza alisema aina hiyo ya ujenzi wa madaraja ni nafuu sana ikilinganishwa na madaraja yanayojengwa kwa nondo na zege.

Alibainisha kuwa ujenzi wa daraja la upinde wa mawe wanatumia makunzi ya mawe na saruji pekee pasipo kuweka nondo na zege, na kubainisha kuwa kama wangetumia nondo na zege lingegharimu zaidi ya sh mil 375.

Aliongeza kuwa daraja hilo ni imara zaidi na litaweza kutumika kwa miaka mingi pasipo kuharibika, ila akatoa wito kwa wakazi wa kata hizo kutopitisha mifugo yao kwenye barabara zinazojengwa katika maeneo yao ikiwemo daraja hilo.

Mhandisi Manyama alieleza kuwa mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na umeanza kutumika pamoja na ujenzi wa vipande 2 vya barabara zinazounganisha daraja hilo pande zote mbili.