May 3, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Daraja la JPM kuchechemua uchumi wa nchi 

Judith Ferdinand na Seleiman Abeid, Timesmajira Online, Mwanza

Imeelezwa kuwa daraja la Kigongo-Busisi (J.P.M),linatarajiwa kuwa suluhisho la usafiri kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa pamoja na kuchechemua uchumi wa taifa.

Daraja hilo ambalo linauwezo wa kubeba tani za 160, utekelezaji wake umefikia asilimia 99 na kazi zilizobaki ni kuweka alama za barabara na kutenganisha maeneo kati ya watembea kwa miguu na  magari  huku  zaidi ya bilioni 700 zitatumika mpaka kukamilika kwake.

Hayo yameelezwa Mei 2,2025  na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji wa Serikali,Gerson Msigwa,wakati wa ziara yake na waandishi wa habari wa mikoa ya Mwanza na Shinyanga ya kumtembelea miradi ya maendeleo.

Ambapo amesema,daraja hilo ni moja ya miradi ambayo inategemewa kuchechemua uchumi wa Tanzania,kupitia ukanda wa Ziwa linalotarajiwa kudumu kwa miaka 100.

“Ukanda huu una uchumi mkubwa ambao unahusisha nchi jirani,kupitia daraja hili tunakwenda kuchechemua uchumi  wa nchi kwa kushirikiana  na  nchi jirani  za Burundi,Rwanda, Congo pia  ni utatuzi wa usafiri kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa ambao wanavuka eneo hili la Kigongo-Busisi, wanapoteza zaidi ya saa nne kwa ajili ya kusubili kivuko,”amesema Msigwa.

Kwa upande wake Msimamizi wa mradi huo kutoka TANROADS Mhandisi William Sanga,amesema,daraja hilo lina urefu wa Kilomita 3 na upana wa mita 28.45  na barabara unganishi  kilomita 1.66 chini ya ufadhili wa Serikali.

Mhandisi Sanga,amesema mradi huo unaunganisha Wilaya ya Sengerema na Misungwi,ulianza Februari 25,2020,umetoa ajira  zaidi ya 30,000, kati ya hizo asilimia 91.9 ni za wazawa na asilimia 8.1 ni wageni na mpaka sasa Mkandarasi amelipwa bilioni 539.

Amesema kulingana na  idadi kubwa ya magari na abiria wanatumia takribani saa mbili au zaidi kuvuka kwa njia ya vivuko,lakini daraja hilo likikamilika watatumia takribani dakika tatu kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Mhandisi Mshauri wa mradi huo,Abdulkarim Majuto,amesema,mradi huo umebakiza asilimia 1,ili ukamilike na kazi zilizobaki ni pembeni ikiwemo sehemu za kupita watu na kazi ndogo ndogo.

Mhandisi Majuto,amesema mradi huo una jumla ya urefu wa Kilomita 4.66 na upana wake una uwezo wa kupitisha magari sita,kwa maana ya gari tatu kutoka upande wa Mwanza kwenda Sengerema na upande wa pili ni gari tatu pia kuna sehemu ya kupita watu yenye urefu wa mita 2.5 kila upande.