April 19, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dar yang’ara tuzo ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu

Na Irene Mark,Timesmajira

WASHINDI 18 kati ya 40 walioingia kwenye 10 bora kila kipengele za Tuzo ya Mwalimu Nyerere ya uandishi bunifu, wametoka jijini Dar es Salaam.Hata hivyo kati ya washindi 12 walioingia tatu bora kwenye kila kipengele ambao walipata zawadi ya fedha taslim, washindi nane wanatoka Dar es Salaam pia.

Kamati ya uandaaji wa tuzo hiyo ulitenga nyanja nne za Ushauri, Riwaya, Tamthilia na Hadithi za Watoto ambazo waandishi bunifu walipeleka kazi zao kushindanishwa.

Akizungumza kabla ya utoaji wa tuzo hizo jijini Dar es Salaam Aprili 13, 2025 Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, Profesa Penina Mlama amesema jumla ya miswada bunifu 282 ilipokelewa kutoka nyanja zote.

Profesa Mlama amesema kamati imefurahi kuona mwitikio mkubwa wa waandishi bunifu kushiriki katika tuzo hizo tofauti na mwaka jana 2024 ambapo kamati ilipokea miswada 209 na miswada 283 iliyopokelewa mwaka 2023 wakati ilipoanzishwa tuzo hizo.

“Kati ya miswada 282 iliyowasilishwa mwaka huu, ya ushairi ilikuwa 114, riwaya 46, hadhiti za watoto 77 na tamthiliya ni 45.

“Hata hivyo kwa mwaka huu jumla ya miswada iliyotimiza vigezo vilivyowekwa ilikuwa ni 205 kati ya 282, naendelea kuwasihi sana waandishi bunifu kuzingatia vigezo vilivyowekwa ili kuepuka kuwasilisha kazi ambazo hazijazingatia vigezo, washiriki wa mwaka huu wametoka katika mikoa yote ya Tanzania na miswada minne imetoka kwa watanzania wanaoishi nje ya nchi,” alisema Profesa Mlama.

Kuhusu ushiriki wa wanawake kwenye tuzo hiyo, mesema walikuwa 88 sawa na aslimia 32 na kwamba hilo ni ongezeko kutoka washiriki 62 mwaka jana huku idadi ya wanaume ikiwa 194 ikilinganishwa na 155 wa mwaka jana.

Profesa Mlama ameendelea kutoa wito kwa washiriki wa tuzo hiyo kuongeza ubunifu na kuzingatia vigezo ili kupata kazi bora zaidi zenye ushindani mkubwa.