Leon Bahati,Timesmajiea,Online
MTAALAMU wa Afya amesema ukimuona mwanao ana dalili za homa pamoja na tatizo la mafindofindo unapaswa kumpeleka hospitali akatibiwe mapema ili kuepuka madhara ya hatari yanayomnyemelea.
“Dalili za ugonjwa huu siyo za kupuuzia hata kidogo,” amesema Profesa Pilly Chillo, ambaye ni mtafiti wa magonjwa anayehudumia katika hospitali ya Taifa ya Taifa ya Muhimbili tawi la Mloganzira.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Profesa Chillo aliutaja ugonjwa huu kuwa ni wa Moyo wa Homa ya Romatiki (RHD).
Alisema ugonjwa huo ukikomaa husababisha uharibifu wa vali (valvu) za moyo ambazo tiba yake ni upasuaji ambao gharama yake ni kubwa na mtu wa kipato cha kawaida hawezi kuimudu.
“Ni ugonjwa unaoongozwa kwa kusababisha upasuaji wa moyo pamoja na vifo vya vijana na hata watu wazima,” ameonya Profesa Chillo.
Akielezea kuhusu RHD, Profesa Chillo alisema ni ugonjwa ambao unaweza kuzuilika na pia anayeugua ni rahisi kutibiwa na kupona kabisa.
Alisema RHD ni ugonjwa unaowashambulia zaidi watoto chini ya miaka 15 kutokana na maambukizi ya mafindofindo yatokanayo na bakteria aina ya Streptococcus.
“Watoto wanaogundulika na homa ya rumatiki, matibabu yake huzuia maambukizi yasiendelee na pia huzuia athari kwenye vali za moyo zisitokee,” alisema.
“Dalili za RHD ni mtoto kuwa na mafindofindo ambayo yanaambatana na homa kali, koo kuuma na sauti kukauka, viungo kuuma na pia kuvimba, matatizo kwenye ngozi na moyo kwenda mbio.”
“Homa ya rumatiki hutokea kati ya wiki ya pili hadi ya nne baada ya mtoto kupata mafindofindo yatokanayo na bakteria aina ya Streptococcus.”
Alisema mgonjwa asipotibia huingia katika hatua nyine ambayo ni kuanza kuathiri vali za moyo hivyo kufanya ushindwe kufanya kazi yake ya kusukuma damu vizuri na kumsababishia mgonjwa kupata dalili kama vile kushindwa kupumua vizuri, kuchoka sana, miguu na tumbo kujaa maji.
Ugonjwa huu, alisema ni tatizo kubwa hapa nchini kwani ndio unaoongoza kwa kusababisha vifo vitokanavyo na matatizo ya moyo kutofanya kazi vizuri kwa watoto na vijana chini ya miaka 35.
Maeneo ya nchi ambayo yameathirika zaidi, Profesa Chillo aliyataja kuwa ni mikoa ya Manyara, Arusha, Singida, Shinyanga na Dodoma.
Hata hivyo, alisema utafiti wao unaonesha kuwa ni ugonjwa ulioenea nchi nzima, hivyo jamii inapaswa kuchukua hatua za kufahamu dalili zake na kuchukua hatua.
Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCDA), Dkt. Samwel Rweyemamu alisema wagonjwa wengi wa RHD wanaofikishwa kwenye hospitali za rufaa kwa tatizo la moyo wengi wao hufanyiwa operesheni ili kuwekewa vali.
Rweyemamu ambaye ni daktari bingwa wa maradhi ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, alisema zinahitajika zaidi ya Sh. 30 milioni kumuwekea mgonjwa wa RHD vali maalumu kumsaidia aendelee kuishi.
Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari wa Tiba ya Moyo Barani Africa (PASCAR), Dkt Emmy Okello alisema kuwa watu milioni 40.5 duniani wana RHD na kati yao 300,000 hufa kila mwaka.
Dkt. Okello ambaye alikuwa akizungumza kwenye mkutano maalumu wa kampeni dhidi ya RHD kwa waandishi wa habari Barani Afrika, alisema bara hili ndilo linaloongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi.
More Stories
Madaktari bingwa wa Samia watua Rukwa
Utashi wa Rais Samia na matokeo ya kujivunia vita dawa za kulevya nchini
Uwekezaji wa Rais Samia sekta ya afya waendelea kuwa lulu Afrika