December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu Mkuu wa (CWT ) akielezea kuhusu mradi wa SITT na kuonyesha zana rahisi ambazo zinaweza kutumika kufundishia wanafunzi bila kuingia gharama

CWT waiangukia Serikali

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma

CHAMA cha Walimu Taifa (CWT) kimeiomba Serikali ikiunge mkono katika mradi wake wa Mafunzo ya Walimu Shuleni (SITT) kwa lengo la kuongeza mbinu rahisi za ufundishaji.

Katibu Mkuu wa Chama hicho, Deus Seif amesema, kama Serikali itawaunga mkono, upo uwezekano wa kufikia walimu katika Mikoa yote kutoka katika Mikoa sita ambayo mradi unatekelezwa kwa sasa na kuonyesha matokeo chanya katika sekta ya Elimu .

“Tunaishukuru Serikali kwa kuruhusu walimu kwenda kwenye mafunzo lakini bado tunaiomba ituunge mkono maana kama tukisema tukae meza moja tukasema CWT bajeti yetu hii hapa, bajeti ya mfadhili na Serikali nayo ikasema na sisi tunaweka mkono, tunaweza kutoka kwenye Mikoa mitatu ikawa sita huenda ikawa Mikoa 12 na baadaye kufikia walimu Mikoa yote,” amesema Seif.

Mratibu wa Mradi huo kutoka CWT, Donatian Marusu amesema, mradi huo umeanza mwaka 2000 kwa majaribio na utekelezaji wake rasmi ulianza mwaka 2012 ambapo hadi sasa tayari mradi umewafikia walimu 10,000 katika Wilaya 21 za Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara.

Mwezeshaji wa mradi wa SITT, Dawite Dukho Sagday akionyesha umbo la pembe nne ambalo mwalimu na mwanafunzi wanaweza kutengeneza kwa kutumia vijiti na mbegu mbichi.

“Hatua hiyo ni kwa awamu mbili, sasa tupo katika awamu ya tatu ya mradi katika Mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora na Shinyanga ambapo tumelenga kuwafikia walimu 3,000 katika Mikoa hiyo kuanzia mwaka jana hadi 2021,” amesema Marusu.

Marusu amesema, utaratibu huo pia unatoa mafunzo kwa walimu wa vyuo vya ualimu ambapo Januari mwaka huu wataalam kutoka Afrika Kusini walitoa Mafunzo kwa wakufunzi na wakuu wa vyuo vya ualimu 24 katika vyuo sita .

Mradi wa SITT, unaelekeza walimu katika shule za msingi kutumia zana rahisi zinazopatikana katika mazingira husika kwa ajili ya kujifunzia kwa vitendo njia ambayo ni rafiki na humwezesha mwanafunzi kuelewa haraka.