Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Tanga
MKUU wa Mkoa wa Tanga Omar Mgumba amesema Benki ya CRDB kwa kuwapa wakandarasi mitaji ya mabilioni ya fedha, itawasaidia kupata kazi ya ukandarasi, na kuweza kushiriki kwenye ujenzi wa miradi mikubwa ya kitaifa.
Amesema wakandarasi wa hapa nchini walikuwa wanashindwa kupata kazi kutokana na ukosefu wa mitaji, sababu ili kupata mkopo ilitakiwa kuwa na dhamana ya fedha ama mali zizizohamishika ikiwemo nyumba, lakini Benki ya CRDB itatoa mikopo hiyo bila dhamana.
Aliyasema hayo Novemba 14, 2022 kwenye semina ya siku moja iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa wateja wake wa Mkoa wa Tanga waliopo kwenye wilaya nane, halmashauri 11 na majimbo 12 ya mkoa huo, na kufanyika jijini Tanga, huku baadhi ya viongozi wa Serikali ngazi ya mkoa na wilaya wakihudhuria.
Mgumba alisema Benki ya CRDB imefanya mageuzi makubwa kwenye kutoa mikopo, kwani kwenye mikopo ya wajasiriamali wadogo, imetoka kuwakopesha wajasiriamali sh. milioni 50 hadi sh. bilioni mbili, huku wakandarasi wakikopeshwa sh. bilioni mbili hadi sh. bilioni 20. Na pindi wakandarasi hao wakiungana watano, wanaweza kukopeshwa hadi sh. bilioni 100.
“Benki ya CRDB imefanya jambo la kipekee nchini kwa kuamua kutoa mikopo kwa wakandarasi nchini bila dhamana. CRDB wanatoa mikopo ya kuanzia sh. biloni mbili hadi bilioni sh. 20 kwa mkandarasi mmoja. Na kama wataungana watano, wanaweza kupewa hadi sh. bilioni 100. Fedha hizi zitawasaidia kupata mikopo na kushiriki ujenzi wa miradi mikubwa kwa kushirikiana na wakandarasi wa nje, kwani walikuwa wanashindwa kushiriki kwenye miradi hiyo sababu walikuwa hawana mitaji.
“Lakini sasa, hata miradi yetu sasa itakwenda kwa kasi sababu fedha za kuwalipa wakandarasi ili iweze kutekelezwa kwa haraka, zipo. Lakini pia, Benki ya CRDB kwa wajasiriamali wadogo na wa kati imetoka kwenye kuwakopesha sh. milioni 50 hadi sh. bilioni mbili. Hilo litawasaidia wakulima, wavuvi na wajasiriamali wengine kunufaika na mikopo hiyo” alisema Mgumba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela alisema kutokana
na Mkoa wa Tanga kuwa mmoja ya mikoa ya kimakakati katika mpango wa biashara wa Benki ya CRDB kutokana na fursa za kiuchumi zilizopo katika mkoa huo, itawawezesha wafanyabiashara na wajasirimali kuweza kuagiza na kuuza bidhaa zao nje ya nchi wakitumia Bandari ya Tanga.
“Kutokana na maboresho yanayofanywa na Serikali kwenye Bandari ya Tanga, na hapa tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa maboresho ya bandari hiyo, sasa wafanyabiashara na wajasiriamali wataitumia Bandari ya Tanga kupitisha mizigo. Hivyo, Benki ya CRDB tutawawezesha wafanyabiashara hao ili waweze kuagiza bidhaa zao nje ya nchi, na sisi kuwawezesha ili waweze kulipia bidhaa hizo.
“Kwa kuwawezesha huko, wataweza kuingiza bidhaa zao kwa wakati, kufanya biashara na kulipa kodi serikalini. Pia kuna fursa nyingine kwenye Bomba la Mafuta, ambapo litawasaidia wafanyabishara, wajasirimali na wananchi kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kuuza chakula, kuku, mayai, maharage na nyama” alisema Nsekela.
Nsekala alisema wameandaa semina hiyo ili kuona wafanyabiashara wa mkoa wa Tanga wananufaika na fursa hizo, badala ya kuwaachia wageni kutoka nchi jirani
More Stories
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi
Kampeni ya Sako kwa Bako yawafikia Kanda ya Kati