June 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CRDB Bunge Grand Bonanza kurindima kesho Dodoma

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

KUELEKEA kuhitimisha Bunge la bajeti kuu ya serikali bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Kwa kushirikiana na benki ya CRDB limeandaa CRDB Bunge Grand Bonanza litakalo fanyika kesho Juni 22,2024.

Akizunguma na waandishi wa habari jijini hapa leo Juni 21,2024,Bungeni Mwenyekiti wa Bunge Bonanza, Festo Sanga amesema kuwa bonanza hilo mbali na kuwa na lengo la kuimarisha afya lakini pia ni kuleta mahusiano kati ya Bunge na Taasisi zingine za umma zitakazoshiriki katika bonanza hilo.

Amesema kuwa Bonanza hilo lililodhaminiwa na Benki ya CRDB litafanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini hapa huku Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ally Mwinyi akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano kutoka CRDB,Tully Mwambapa amesema kuwa benki hiyo imekuwa ikishirikiana kwa ukaribu na wabunge ambapo wamekuwa wakitoa huduma mbalimbali za kibenki pamoja na kudhamini mabonza ya kimichezo.

“Licha ya kushirikiana na serikali katika uwekezaji kwenye elimu,afya na mazingira lakini tumekuwa tukidhamini mabonanza ya kimichezo yenye lengo la kuimarisha afya na katika bonanza hili tumedhamini vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 85 huku udhamini wa bunge grand bonaza kwa ujumla ni shilingi milioni 266,”amesema Mwambapa.