November 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CRA yafungia Clouds Redio na TV siku saba

Wasimamizi wa ma-group ya Whatsaap, watumiaji wa mitandao nao watakiwa kuzingatia matakwa ya sheria kuhusu uchaguzi wanapohusisha mitandao

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imefungia Kituo cha redio na televisheni vinavyomilikiwa na Kampuni ya Clouds Media Group kwa kukiuka Kanuni za Utangazaji masuala ya uchaguzi kwa muda wa siku saba.

Kwa uamuzi huo, adhabu hiyo itaanza kutekelezwa kuanzia kesho Agosti 28 hadi Septemba 3, mwaka huu. Uamuzi huo umetangazwa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema kituo hicho kimekiuka sheria kwa kutangaza matokeo ya kupita kwa wabunge bila kupingwa, hivyo kinatakiwa kutorusha matangazo yoyote kuanzia leo saa nane mchana hadi keshi asubuhi, isipokuwa yapitishwe matangazo ya kuomba radhi kwa Watanzania.

Sambamba na kufungiwa kuanzia leo na kesho kazi ya vituo hivyo iwe ni kuomba radhi umma wa Watanzania kwa kitendo walichokifanya. Aidha, alisema katika kipindi cha 360 na Power Breakfast kituo hicho kilirusha takwimu za wagombea ubunge waliopita bila kupingwa, huku taarifa hiyo ikiwa haijathibitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CNEC), hivyo kukosa mezania.

Mhandisi Kilaba alimnukuu mtangazaji mmoja wa kituo hicho akisema; “Sasa kuna wagombea ambao wamepita bila kupingwa …mimi nilikuwa ninazo 23 mpaka saa hizi (kumi na nane zikaongezekaje hizo zingine)…si watu wanazidi ku-confirm (kwa hiyo kuna uwezekano kwamba zinaweza kuzidi)…zinaweza kuzidi.

“Ishapita kwa sababu, aaah mpaka saivi tunaingia mtamboni hapa …23 washafika.”

Ameisema kifungu cha 16 (1) cha kanuni za Utangazaji (Maudhui) na kanuni ndogo za utangazaji wakati wa uchaguzi za mwaka 2015 zimebainisha wajibu wa mtoa maudhui kutoa taarifa za matokeo ya uchaguzi kwa kadri zinavyopatikana na kutolewa na NEC na kuhakikisha matokeo yanatangazwa kwa ufasaha .

Mhandisi Kilaba amesema mtoa huduma ya maudhui anapaswa kufuata kanuni, sheria na masharti ya leseni sambamba na maelekezo yanayotolewa na mamlaka .

“Imejidhihirisha wazi kuwa vituo vingi vya utangazaji vina leseni, lakini havisomi masharti ya leseni hizo na kuhakikisha uhai wa leseni zao.

Kanuni ya leseni za mawasiliano ya 39(2) inavitaka vituo vya utangazaji kutuma maombi ya kuhusisha leseni zao mwaka mmoja kabla muda wa leseni kumalizika,” amesema.

Mhandisi Kilaba alivitaka vyombo vya utangazaji kuzingatia kanuni hizo ili ziwawezeshe kutangaza masuala ya uchaguzi kwa weledi na kudumisha amani ya nchi.

Pia aliwataka watumiaji wa mitandao ikiwemo ya kijamii hususani wasimamizi wa makundi (admin) na wanachama wa vyama vyote vya siasa kuzingatia matakwa ya kisheria kuhusu masuala ya uchaguzi wanapohusisha mitandao ya mawasiliano.