November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CPA.Makalla auunguruma Ubungo

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online Dar.

KATIBU wa NEC, Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Taifa na Mlezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar-es-Salaam, CPA.Amos Makalla, leo Julai 14, 2024 ameendelea na ziara yake ya siku 10 mkoani Dar-es-Salaam, kwa kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo Wilaya ya Ubungo ambapo ameanza na Jimbo la Kibamba na kumalizia Ubungo.

CPA Makalla amekagua miradi ya maendeleo ikiwa pamoja na shule ya kisasa ya mchepuo wa Sayansi ya Wasichana kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha sita (Dar-es-Salaam Girls High School ) iliyopo Kata ya Kwembe Wilaya ya Ubungo, iliyogharimu bilioni 4 .

Huku mradi mwingine ukiwa wa tenki la maji lenye ujazo wa lita 6000 lilipo eneo la Mshikamano, Jimbo la Kibamba Wilaya ya Ubungo.

Awali Ofisa Elimu Wilaya ya Ubungo, Voster Mgina, akisoma taarifa yake kuhusu shule hiyo wa wasichana ya Dar-es-Salaam mbele ya Mwenezi Makalla amesema, shule hiyo ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 1000 ikiwa na madarasa 20.

Hivyo itasaidia kupunguza msongamano kwa wananfunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita katika shule hiyo, huku akisema mradi huo umefikia asilimia 99 ya utekelezaji wake.

Pia amesema walikutana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mkandarasi kukimbia na kuacha mradi kutokana na za miundombinu ya barabara.

Kwa upande wake CPA Makalla, ameonesha kufurahishwa kwa uwepo wa miradi hiyo ya maendeleo huku akieleza kuwa Rais Dkt.Samia ametoa fedha kwa kila Mikoa kujenga shule yenye hadhi kama hiyo ambayo kwa Mkoa wa Dar es salaam ndio peke huwezi kufanannisha na shule nyingine kama Zanaki, Forodhani wala Jangwani.

Hata hivyo, Makalla ametumia nafasi hiyo kumtama Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo kusimamia vizuri wanafunzi hao kwani yeye ndio chachu huku akiwataka wanafunzi kutokuwa watoro na kubeba mimba badala yake wasome kwa bidii na kuleta matokeo mazuri ambayo yafanane na hadhi ya shule hiyo.

“Kiukweli natoa pongezi kwa Rais kuwekeza kwa wananchi wake, tukianza na shule hii ni ya mfano kwa Mkoa wa Dar-es- Salam na Tanzania nzima kwa ujumla hivyo kazi iliyobaki ni kwenu wanafunzi na walimu kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,”amesema Makalla.

Katika mradi wa maji, ameitaka Mamlaka ya Maji Safi na Usafiri wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), kuhakikisha wanafikisha huduma ya maji pembezoni mwa Jiji hilo huku akibainisha kuwa kutofanya kwao vizuri ni kuwagombanisha wananchi na CCM.

“Mradi huu wa maji ni mzuri na nimefurahishwa nao, hivyo niwaombe DAWASA kuhakikisha mnafikisha Maji pembezoni mwa Jiji la Dar es salam kwani wananchi, wanaimani kubwa na CCM mnapofanya vibaya mnawagombanisha wakati RaisSamia ameishafanya utekelezaji kazi imebaki kwenu kufikisha maji kwa wananchi wa Jimbo la Kibamba na Wilaya ya Ubungo kwa ujumla,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa Mradi Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar-es-Salaam (DAWASA), Ramadhani Mtindasi, amesema eneo la Msumi ndio halina huduma ya maji.

Aidha Mtindasi amesema wanampango wa muda mrefu wa kusambaza maji kwa kuchimba visima 3 ambayo vitasaidia kupunguza changamoto ya kukosa huduma ya maji kwa baadhi ya maeneo.