November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yataka huduma za msingi zielekezwe hospitali ya Wilaya Ilemela

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza CPA Amos Makalla amezitaka taasisi za umma kama vile MWAUWASA, LATRA, TANESCO kuhakikisha wanatoa kipaumbele katika utoaji wa huduma za msingi katika hospitali ya Wilaya ya Ilemela ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi

Makalla ametoa maelekezo hayo alipofika katika hospitali ya Wilaya ya Ilemela kwa ajili ya kukagua ukamilishaji wa miundombinu ya hospitali hiyo.

Akitoa maelekezo hayo ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA) kujiridhisha na uwepo wa huduma ya maji ya uhakika katika hospitali ya Wilaya pamoja nakutoa kipaumbele ili huduma ziweze kutolewa kwa uhakika na ubora.

“MWAUWASA mjiridhishe juu ya utoaji wa huduma ya maji katika hospitali hii ya Wilaya na utoaji wa maji uwe wa uhakika na hospitali hii ipewe kipaumbele, watumishi hawataweza kufanya kazi vizuri kama hakuna huduma ya maji ya uhakika,”amesema Makalla.

Pia ameitaka LATRA,Ofisa Usafirshaji Mkoa na Wilaya kuhakikisha magari yanafika .katika hospitali hiyo ya Wilaya ili kuwarahisishia wananchi usafiri wa kufika kwa ajili ya kupata huduma na kumtaka Mkuu wa Wilaya kusimamia utekelezaji wa agizo hilo.

“Nimekagua ujenzi wa barabara,nimeona jiografia ya huku, naamini itarahisiha wananchi kuja huku, maelekezo yangu LATRA, Ofisa usafirishaji Mkoa na Wilaya kuweka utaratibu wa magari yanayotakiwa kufika huku ili kuwarahisishia wananchi kufika hospitali ya wilaya na kupata huduma,”.

Ametumia nafasi hiyo kuwapongeza watumishi wa idara ya afya kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuhudumia wananchi huku akiwahimiza kusimamia na kuitimiza dhamira ya Rais ya kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Dkt. Samson Marwa amesema kuwa kwa sasa hospitali hiyo ya Wilaya inatoa huduma kwa wagonjwa wa nje tu (OPD).

Ambapo tangu ianze kutoa huduma mwaka 2020 hadi 2023 imeshahudumia jumla ya wagonjwa 7079 na akaongeza kuwa itakapokamilika kwa asilimia 100 itarahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa maeneo ya Wilaya ya Ilemela na maeneo jirani.