Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
WATANZANIA 100 walioondoka nchini kinyume cha sheria na kuzamia nchini Afrika Kusini, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la kuondoka nchini bila kufuata taratibu za Uhamiaji.
Watuhumiwa hao, ambao wengi ni vijana wamesomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mahakama Kisutu, Thomas Simba jijini Dar es Salaam jana. Washtakiwa wote walikiri kutenda kosa hilo na wameomba mahakama iwasamehe.
Hata hivyo, Hakimu Simba amesema kuwa haoni faida yoyote ya kuwapeleka watuhumiwa hao gerezani hasa katika kipindi hiki ambacho kuna ugonjwa hatari la Corona.
“Sioni faida yoyote ya kuwapeleka gerezani lakini mahakama inawapa onyo kali na inawaachia kwa masharti msirudie kutenda kosa hili kwa miezi sita,” amesema Hakimu Simba.
Mapema wakisomewa shtaka lao na wakili wa Serikali kutoka Uhamiaji Godfrey Ngwijo, walidai Julai 3, 2020 katika uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere uliopo Ilala jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote 100 walikutwa wakiwa wameondoka nchini kinyume cha sheria bila kufuata utaratibu.
Wakisomewa Maelezo ya awali ilidaiwa katika tarehe zisizojulikana washtakiwa hao waliondoka nchini bila kufuata utaratibu na kwamba Julai 3 mwaka huu watuhumiwa walirudishwa nchini Tanzania baada ya uchunguzi na kugundulika kuwa ni wahamiaji haramu.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja