March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira

Ofisa Biashara Mwandamizi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Clara Mwamba, amesema Maonesho ya 50 ya Jubilee ya Sabasaba yanayotarajiwa kufanyika mwaka 2026 yatakuwa ya kipekee kutokana na Tantrade kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwa maonesho hayo makubwa ya biashara nchini.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam na TimesMajira katika kuelekea maadhimisho ya maonesho hayo, Mwamba amesema mwaka huu kutakuwa na maboresho mbalimbali ikiwemo uboreshaji wa mabanda ya maonesho pamoja na uwepo wa programu maalumu zitakazoenzi historia ya Tantrade.

Amesema maonesho ya Sabasaba yameendelea kuwa jukwaa kubwa la biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki, yakitoa fursa kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kukutana, kubadilishana uzoefu na kupanua masoko.

“Katika maonesho ya mwaka huu tutayaenzi na kujivunia kwa sababu ni ya kipekee, tukisherehekea miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Tantrade. Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Maonesho ya Kimataifa ya Dar es Salaam: Fahari ya Tanzania,’” amesema Mwamba.

Amesema ndani ya kipindi cha miaka 50 ya maonesho hayo, mafanikio makubwa yamepatikana ikiwemo kuongezeka kwa ajira, kupatikana kwa masoko ya ndani na nje kwa bidhaa za Tanzania pamoja na kukuza sekta binafsi.

“Maonesho haya yameongeza chachu ya ukuaji wa masoko ya bidhaa za Tanzania na kufanya biashara kukua maradufu ukilinganisha na miaka ya nyuma,” ameongeza.

Mwamba pia alieleza kuwa Serikali imekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha maonesho hayo kupitia uboreshaji wa miundombinu, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

Aidha, amesema Tantrade inalenga kuvutia makampuni mengi zaidi kutoka nje ya nchi ili kuongeza ushindani na kuleta teknolojia mpya pamoja na ujuzi ambao wafanyabiashara wa Tanzania wanaweza kujifunza.

“Makampuni ya kimataifa yanapokuja hapa yanakuja na teknolojia na utaalamu. Hivyo wafanyabiashara wa Tanzania wanapata nafasi ya kujifunza na kuboresha biashara zao,” amesema.

Kwa mujibu wa Mwamba, mwaka huu Tantrade imejipanga kuvutia nchi nyingi zaidi kushiriki katika maonesho hayo ya Jubilee ya miaka 50, huku sekta zitakazopewa kipaumbele katika uwekezaji zikiwa ni viwanda vinavyoongeza thamani ya bidhaa, teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), miundombinu pamoja na nishati mbadala.

Amesema maonesho ya Sabasaba yameendelea kuwa daraja muhimu la kukuza biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kimataifa kwa manufaa ya uchumi wa Tanzania.