Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Dar
KAMPUNI ya Heritage Drinking Water imeendelea na uzinduzi wa huduma ya maji ya kunywa ambapo kwa sh. 200 mtu anapata chupa yenye na maji ya ujazo wa lita moja lengo likiwa ni kuwawezesha Watanzania kushiriki kutunza mazingira, huku wakiokoa pesa.
Uzinduzi huo umefanyika mwishoni mwa wiki Chuo Kikuu Ardhi, jijini Dar es Salaam, huku kauli mbiu ya mradi huo ikiwa ni Okoa Mazingira, Okoa Pesa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo Chuo Kikuu Ardhi, mgeni rasmi Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Makongo, Saida Mbatta, amesema hatua hiyo ya Kampuni ya Heritage Drinking Water ni utekelezaji wa vitendo wa Sera ya Taifa ya ujenzi wa viwanda.
Mbatta amesema pamoja na miradi ya maji inayotekelezwa na Serikali, bado hitaji la maji nchini ni kubwa.
Ametolea mfano takwimu za kimataifa zinazoonesha kuwa ifikapo mwaka 2025, hitaji la maji litazidi kuwa kubwa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Hivyo amepongeza Kampuni ya Heritage Drinking Water kwa hatua hizo, kwani wanazidi kutengeneza ajira, wamekidhi matakwa ya viwango kama inavyoelekezwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), wamesogeza huduma karibu na wateja, bei ya maji inaendana na hali halisi ya mwananchi wa kipato cha chini, wanakidhi hitaji la maji kwa kiwango kikubwa .
Ametoa mwito kwa kampuni hiyo kusambaza zaidi huduma hiyo, kutangaza mradi huo ili watu wa hali ya chini waweze kupata huduma hiyo.
Akizungumzia kuzinduliwa kwa mradi huo chuoni hapo, Waziri wa Malazi na Huduma wa Chuo Kikuu Ardhi, Ndalingwa Ibrahim, amesema mradi huo kupelekwa chuoni hapo ni fursa kubwa sana na utawasaidia kuokoa fedha zao.
Amesema badala ya kununua chupa ya lita moja kwa sh. 500, lakini Heritage inawawezesha kupata maji na chupa ya kudumu kwa sh. 200, hivyo mradi huo utawasaidia sana.
Mmoja wa wakurugenzi wa Kampuni ya Heritage Drinking Water, Dkt. Edwinus Lyaya, amesema; “Tumekuja na mradi huu lengo kubwa likiwa ni kutunza mazingira.
“Tunatunzaji mazingira; Tuna chupa zetu za kudumu ambazo mtu akiitumia atapata maji ya kunywa. Ni chupa nzuri anaweza kuingia nayo sehemu yoyote na maji yakiisha anakuja analipia na kuwekewa au kujiwekea maji kwa gharama ya sh. 200 kwa lita.
Maana yake hatuchafui mazingira kwa sababu kazi hii ya uokozi wa mazingira si nyepesi, ndiyo maana tumeona maji haya yasiwe gharama kubwa sana, yawe ni gharama ya kawaida, ndiyo maana tunayauza kwa sh. 200 kwa lita moja ili mtu aweze kuokoa pesa zake kama motisha ya kutunza mazingira.”
Dkt. Lyaya amesema huo ni utaratibu mpya ambao wanaujenga katika nchi yetu ili baadaye ukishazoeleka mtu anaweza kutunza mazingira kwa njia hiyo.
Hata hivyo, Dkt. Lyaya amesema kama mtu ana chombo chake cha maji anaweza kufika sehemu yanakopatikana maji hayo, akapata maji mengine kwa kutumia chombo chake chochote, hivyo mtu hawezi kuchafua mazingira kwa kutupa chupa hovyo.
“Hilo ndilo wazo kubwa ndiyo maana tukaja na kauli mbiu ya mradi huu ya Okoa Mazingira, Okoa Pesa,” amesema na kuongeza kuwa huduma kama hizo zimeishazinduliwa maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Ametaja maeneo hayo kuwa ni Hosteli ya Mabibo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS), Soko Kuu Kariakoo, Simu 2000 Mawasiliano, Tegeta Nyuki, Ilala Sokoni na Tandika Sokoni.
Kupitia majokovu yanakopatikana maji hayo mtu anajihudumia kupitia kadi maalum au kwa kutumia noti au koini.
Akieleza kazi zinazotekelezwa na kampuni hiyo, Dkt. Lyaya alisema wanafanyakazi mbalimbali kama kampuni, ikiwa ni pamoja na kusafisha fukwe, mazingira katika Jiji la Dar es Salaam na wanafanyakazi za utafiti wa kimazingira.
“Lakini kwa kiasi kikubwa kampuni imesaidia kuondoa mifuko ya rambo jijini Dar es Salaam na tuna cheti cha mazingira kutoka Baraza la Taifa la Mazingira NEMC cha kutambua mchango wetu,” amesema, Dkt. Lyaya.
Amesema baada ya tatizo la rambo wao kama kampuni wamekuwa wakifikiria namna ya kukabiliana nalo na changamoto nyingine za mazingira.
Kwa mujibu wa Dkt. Lyaya tatizo sugu ni la uchafuzi wa mazingira kwa chupa tupu za maji. “Mtu anakunywa maji, akimaliza ile chupa anatupa, hatuna miundombinu za kuhifadhi chupa za maji na nyingine na ni wazi nyinyi ni mashahidi huko mitaani hali ikoje,” alisema.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam