December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chuo cha Mweka kufungua tawi Iringa

Na Mwandishi wetu,timesmajira

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt Pindi Chana, amekiagiza Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka, kuanza rasmi kutoa Mafunzo Mkoani Iringa ili kuwajengea uwezo wadau wa utalii katika mikoa ya kusini.

Waziri Balozi Dkt Pindi Chana ameahidi, kusaidia mchakato wa uanzishaji wa Kampasi ya Chuo katika eneo la Kihesa Kilolo Mkoani Iringa.

Agizo hilo limefuatia ombi lililotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendegu wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Kimataifa ya UTALII KARIBU KUSINI yaliyofanyika Kilolo Mkoani Iringa.

Mkuu huyo wa Mkoa amemuomba Waziri asaidie Chuo cha Mweka kiweze kutoa mafunzo na kuanzisha Kampasi kama moja ya mkakati wa kukuza utalii katika mikoa kumi ya kusini.

Naye Mkuu wa Chuo cha Mweka, Profesa Jafari Kideghesho, amesema kuwa Chuo kiko tayari kutekeleza agizo la Waziri kwa kuwa tayari kupitia mradi wa REGROW, unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, Chuo kimetengewa ardhi yenye ukubwa wa ekari 50 katika eneo la Kihesa wilayani Kilolo lengo la Mradi wa REGROW ni kukuza utalii kusini mwa Tanzania, hususan katika mikoa kumi ya kusini ambayo ni Morogoro, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Ruvuma, Rukwa, Katavi, Lindi na Mtwara. “Tuna wanataaluma wa kutosha ambao ni wabobezi katika masuala ya uhifadhi na utalii pamoja na vitendea kazi vya kutosha kutekeleza agizo la Mheshimiwa Waziri”, amesema Profesa Kideghesho.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt Pindi Chana, akicheza ufunguzi wa Maonesho ya Kimataifa ya UTALII KARIBU KUSINI yaliyofanyika Kilolo Mkoani Iringa.

Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, amemshukuru Waziri akisema kuwa agizo la Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii kwa Chuo cha Mweka limekuja wakati muafaka kutokana na unyeti wa Sekta ya Utalii . “Utalii makini unahitaji wataalamu wenye weledi, ujuzi na mitizamo sahihi. Hivyo, suala la mafunzo haliepukiki,” Amesema.

Wananchi wa Iringa na wadau wa utalii wamefurahishwa na agizo hilo la Serikali na utayari wa Chuo cha Mweka kufungua Kampasi katika mikoa ya Kusini wakisema kuwa ni fursa waliyokuwa wanaisubiri kwa miaka mingi. “Mikoa ya kusini ina rasilimali na vivutio lukuki. Bahati mbaya, tofauti na ukanda wa Kaskazini, wakazi wa ukanda wa Kusini hawajanufaika na vivutio hivi huku Serikali ikikosa mapato ya kutosha kutokana na maendeleo duni ya miundombinu na elimu ya utalii. Kampasi ya Chuo cha Mweka hapa Iringa itafungua ukurasa bmpya kwa maendeleo ya utalii na maisha ya wananchi katika mikoa ya Kusini. “Tunamshukuru Samia Suluhu Hassani kwa kuziona fursa zilizoko Kusini na kutoa maelekezo ya kuwepo kwa mazingira rafiki yatakayoruhusu wananchi kunufaika na fursa hizi.” amesema Mwampamba ambaye ni Balozi wa Utalii nchini.