November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chongolo:kufungia maduka kulikuwa kunaleta uadui kwa serikali na wafanyabiashara

Na Zena Mohamed, Timesmajira online, Mpwapwa

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Daniel Chongolo ameipongeza Wizara Fedha na Mipango kwa Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 iliyosomwa jana Bungeni ambapo amesema imejikita katika kutatua changamoto zaidi.

Chongolo amesema hayo Wilayani hapa leo Juni 16,2023 wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kingiti, Kata ya Kingiti ikiwa ni muendelezo wa Ziara yake ya kutembelea majimbo yote yaliyopo Mkoa wa Dodoma ambapo amesema kuwa Bajeti hiyo imegusa jambo kubwa la zuio kwa Taasisi yoyote ya serikali kufunga biashara kwani lilikuwa linaleta uadui.

“Kulitokea wimbi la watu akiamka asubuhi anaamua tu kwenda kufunga biashara ya mtu wewe mtu unatakiwa kufanya biashara ili upate kulipia hicho mtu anachokitaka halafu ili adai anaenda kuifunga biashara sasa unakwenda wapi kutoa pesa,

“Ukifunga biashara maana ake umeniambia nikose hata hicho unachokuja kunidai badala ya kuweka makubaliano ikifika tarehe fulani ulipe unafunga na mtu hana uwezo wa kupata fedha lile jambo siyo zuri,

Amesema amefurahishwa na zuio hilo kwani jambo hilo ilikuwa linajenga uadui kati ya serikali ,taasisi za serikali na wafanyabiashara kwani ni suala la kuzungumza na kukubaliana na siyo kwenda kufungia watu biashara.

“Bajeti imejielekeza huko na maelekezo ya kibajeti kwamba ni marufuku sasa biashara kufungwa kwasababu ya jambo lolote linalozungumzika linakuwa la msingi sana,”amesema Chongolo.

Aidha amesema kuwa bajeti hiyo imebeba dhamira ya dhati ya kubeba uchumi wa Nchi hivyo inatoa fursa ya nchi kusonga mbele kutoka tulipo.

Amesema kuwa bajeti imebeba mambo makubwa na mazuri likiwemo suala la kulinda viwanda vya ndani,utoaji wa mikopo kwa ngazi ya elimu ya kati,kuondolewa kwa tozo za simu pamoja hilo suala la kuondoa zuio la kufunga biashara.

Akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/24 bungeni jana Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba katika mambo aliyowasilisha moja wapo aliyopendekeza kwenye hotuba yake kwamba kuanzia Julai 1,2023 iwe ni marufuku kwa Taasisi yoyote ya Serikali kufunga biashara,Ofisi ama maeneo yoyote ya uzalishaji kwa kigezo cha kukiuka taratibu mbalimbali.