January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chongolo awaweka mtegoni makatibu wa CCM

Na Heri Shaaban, TimesMajira Online, Kigamboni

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, amewaweka mtegoni makatibu wa CCM watakaoshindwa kusimamia mali za chama Cha Mapinduzi.

Katibu Mkuu Daniel Chongolo amesema wakati wa kuzungumza na wanachama wa CCM na Viongozi wa chama hicho baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba ya katibu wa mkoa wa Dar es Salaam inayojengwa Kigamboni pamoja na kuweka jiwe la Msingi Ofisi ya CCM Wilaya Kigamboni Alisema atawachukulia hatua dhidi ya watendaji wanaoshindwa kusimamia mali za chama cha Mapinduzi CCM kwa kushindwa kusimamia .

Akizungumza Oktoba 22,2022 baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba ya katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam na jengo la CCM Wilaya ya Kigamboni, Chongolo, amesema kasi ya kutafuta nyaraka za kisheria za umiliki wa maeneo ya chama imepungua.

“Inasikitisha kuona mali ambazo tumezimiliki kwa miaka mingi mtu anajitokeza na kusema eneo lake , wenye mali ambao ni chama ngazi husika wanatakiwa kusimamia wapo, wamekaa kimya na baadhi wameacha na kuona si sehemu ya wajibu wao tutakapoanza kuchukua hatua zitaelekezwa kwa mtendaji wa eneo husika,” amesema Chongolo.

Awali chama cha Mapinduzi CCM 2017 kiliunda Tume iliyokuwa na jukumu kufatilia Mali za chama kote nchini baada kukabidhiwa ripoti na mambo mengine kilielekeza zitafutwe nyaraka za kisheria za umiliki wa baadhi ya maeneo .

Wakati huohuo katika hatua nyingine Chongolo amekemea tabia ya baadhi ya watu wanaoendeleza rushwa katika uchaguzi na kusababisha wenye dhamira ya kweli ya uongozi kukosa nafasi.“Chama hiki kina watu wazuri wa kuwa viongozi, tatizo ni baadhi yetu kutengeneza miundombinu haramu ya kuwadhibiti watu wazuri kupata uongozi.

“Tutapitia kila jina, tutapitia maelezo binafsi ya kila mgombea na tutajiridhisha ili tupate viongozi wenye dhamira ya kweli ya kuendeleza utumishi wa chama chetu kisonge mbele.

“Vikao vitakavyoenda kuketi Dodoma vitatenda haki, vitafanya kazi bila upendeleo, wale mtakaobakia msitengeneze nongwa, chama kina nafasi nyingi msipate shida…usipotosha leo utatosha kesho,” amesema Chongolo.

Kuhusu ujenzi huo Chongolo amewapongeza viongozi na wanachama kwa kujitoa na kuwataka wajitahidi kukamilisha haraka Ujenzi wa nyumba ya katibu wa mkoa ulianza Juni mwaka huu na mpaka sasa Sh milioni 90 zimetumika na wanatarajia itakamilika Desemba mwaka huu.

Kwa upande jengo la CCM Kigamboni, Katibu wa CCM Wilaya ya Kigamboni, Stanley Mkandawile, amesema ujenzi ulianza mwaka 2020 na mpaka sasa fedha zilizotumika ni Sh milioni 190.7 na kwamba zinahitajika Sh milioni 95.3 kuukamilisha.

Katika hafla hiyo Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndungulile, amemuomba Chongolo kuweka msukumo kwenye Mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam (DMDP) ili waweze kupata barabara kabla ya 2025.

“Tunaomba pia tuangalie upya tozo za daraja, watu wanasema Kigamboni unaingia kwa fedha unatoka kwa fedha,” amesema Dk. Ndungulile.

Katibu wa chama Cha Mapinduzi CCM Taifa Daniel Chongolo(katikati) akikata utepe wakati wa kuweka jiwe la Msingi Ofisi ya CCM WIlaya Kigamboni pamoja na nyumba ya Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam leo Octoba 21/2022 (kushoto)Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam Mama Kate Kamba.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa Dar Es Salaam Mama Kate Kamba akisalimiana na Mkurugenzi wa kampuni ya Wahenga Aluminum John Ryoba Wilayani Kigamboni leo katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM Taifa Daniel Chongolo