May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CPB kuanza kuzalisha kuni kupitia pumba za mpunga

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

BODI ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB),imesema ina mpango wa kuzalisha kuni kupitia pumba za Mpunga ili kupunguza uharibifu wa mazingira.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo  Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB),Dkt. Anselm Moshi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Utekelezaji wa majukumu ya Bodi hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Dkt. Moshi amesema kuwa kwasasa wapo katika upembuzi yakinifu katika kuongeza thamani mazao ya mpunga  ili kuweza kuzalisha mafuta yatokanayo na pumba za mpunga.

“Pia tunampango wa kuanza kutumia teknolojia ya kuzalisha mafuta ya kupikia yatokanayo na pumba za mpunga kupitia kiwanda chetu kilichopo Mkuyuni jijini Mwanza,”amesema.

Aidha,amesema kuwa kwa Mwaka 2021/2022 wamenunua mazao Tan Elfu 26,665,000 yenye Thamani ya shillingi Billion 14.8 na kuongeza Thamani mazao Tan 16,000.3 yenye Thamani Billion 8.2.

Hata hivyo Dkt.Moshi amesema kuwa CPB imedhamiria kuwafikia wakulima wengi zaidi ili wazalishe kwa ufanisi shambani.

“Bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko PCB dhamira yake ni kuwawezesha wakulima kulima kwa kutumia mbinu za kisasa kwa maslahi yao binafsi na Taifa kwa ujumla,”amesema

Dkt. Moshi amesema kuwa ili mkulima apate mapato mengi anatakiwa kulima kwa Tija na kuendana na soko la kibiashara.

“Ikumbukwe kuwa  Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB),  ni Taasisi ya serikali chini ya wizara ya Kilimo iliyopewa dhamana ya kufanya biashara ya nafaka na mazao mchanganyiko na  imeanzishwa kwa sheria ya nafaka na mazao changanyiko Namba 19  ambapo pia hadi sasa mzunguko wa biashara katika taasisi hiyo umeongezeka kutoka bilioni 15 hadi bilioni 52,”amesema Dkt.Moshi.