November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chongolo awataka wananchi kutokubali fidia ya fedha

Na Zena Mohamed, Timesmajira Online, Mpwapwa

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Daniel Chongolo amewataka wananchi wa Kata ya Ng’ambi Wilayani Mpwapwa kutokubali fidia ya fedha na badala yake wachukue fidia ya ardhi kwa maendeleo ya muda mrefu.

Amewataka kukubali kupewa ardhi kwasababu wanapewa kwenye maeneo yenye miundo mbinu hivyo ni rahisi kuendeleza shughuli zao hasa za kilimo.

“Msikubali kupewa fedha,fedha mnatumia inaisha lakini ardhi unaendelea kuwa nayo muda mrefu na mnapewa sehemu zenye miundombinu,”amesema.

Chongolo ameyasema hayo,Wilayani Mpwapwa leo Juni 17,2023 ikiwa ni muendelezo wa ziara yake katika Majimbo yote mkoa wa Dodoma ambapo alitembelea mradi mkubwa wa bwawa la Msagali lililopo Kata ya N’gambi linalojengwa kwa zaidi Shilingi Bilioni 27 akiwa anaelekea Wilaya ya Kongwa baada ya kumaliza ziara yake katika majimbo ya wilaya ya Mpwapwa.

Vilevile amewaasa wananchi kuacha kuuza maeneo yao yaliyo karibu na mradi huo kwa manufaa yao ya sasa na baadae.

“Kuna baadhi ya watu wanajitokeza sasa hivi kuja kuwalaghai ili muuze maeneo yenu kwakuwa wanajua faida itakayopatikana hapa baadae msiwauzie maeneo yenu,”amesema.

Kutokana na hilo amewaagiza viongozi wa eneo hilo kudhibiti ulanguzi wa ardhi unaofanywa na baadhi ya watu kwa wananchi wa eneo hilo.

Mradi huo wa Bwawa la Msagali unaogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 27 linatarajiwa kujazwa maji lita Bilioni 93 ambazo zitasaidia katika shughuli za kiuchumi na Kijamii.

Ambapo Chongolo amesema mradi huo ukikamilika utasaidia katika shughuli za kilimo cha umwagiliaji,ufugaji na binaadamu, hivyo wananchi wapewe fidia ya ardhi karibu na mradi huo ili wanufaike nao.