December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chongolo awataka viongozi Kuwajibika kwa wananchi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Daniel Chongolo amewataka Viongozi wenye dhamana kwenye maeneo hasa watendaji wa halmashauri wanawajibu wa kuwajibika kwa wananchi.

Katibu Mkuu ameyasema hayo jana alipokutana na wafanyabiashara wa soko la Nyanya Ilula ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kukagua na kusimamia Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.

“Ni lazima mjue suala la uwepo wenu ni utumishi na sio vinginevyo, ni kutumikia wananchi na si vinginevyo, ni kutatua changamoto za wananchi na si vinginevyo, tukienda tofauti na hivyo tutakuwa tunaulizwa maswali kila siku bila sababu” amesema Chongolo.

Pamoja na mambo mengine Katibu Mkuu amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Kilolo kusimamia uchaguzi wa kutafuta viongozi wa soko hilo la nyanya.

Soko hilo ambalo limekuwa na ugomvi baina ya makundi mawili yanayogombea uongozi, kutokuwa na choo salama na pia kulalamikiwa juu ya ubadhilifu wa fedha.

Katibu Mkuu ameambatana na Wajumbe wawili wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Katibu wa NEC Oganaizesheni Ndugu Issa Haji Ussi Gavu pamoja na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Ndugu Sophia Mjema.