January 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chongolo atoa maelekezo mradi wa vijana ukamilike Agosti mwaka huu

Na Zena Mohamed, Timesmajira Online ,Mpwapwa

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo ameagiza miradi ya ujenzi wa mabwawa ya umwagiliaji yatakayotumika katika mradi wa mashamba makubwa ya kuwawezesha vijana (BBT) kukamilika ifikapo Agosti mwaka huu.

Amesema anataka miradi hiyo ikamilike haraka ili matokeo yaliyokusudiwa yaanze kuonekana hususan kwa kundi kusudiwa la vijana.

Chongolo ametoa agizo hilo Wilayani hapa leo,June 17,2023 alipotembelea kukagua mradi wa ujenzi wa bwawa la umwagiliaji Msagali ambalo zaidi ya Kaya 10,000 zitanufaika na mradi huo kupitia mashamba makubwa ya umwagiliaji.

Ambapo amemtaka Mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huo ili msimu ujao wa mvua maji yaanze kuingia bwawani kwani hadi sasa amefikia asilimi 49 kwa kipindi cha miezi sita huku akisema mradi huo ufikie angalau asilimia 52.

“Tunataka ifikapo Agosti mwaka huu miradi yote ya kilimo ya vijana iwe imekamilika, matokeo yaonekane,

“Mradi huu ni wa bilioni 27.9 hakutakuwa na maana fedha nyingi hivi zitumike halafu mradi usionyeshe tija, tunataka kuona tija,”amesema.

Aidha amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kufanya mapinduzi makubwa ya kilimo kwa kuhakikisha upatikanaji wa maji ya umwagiliaji na kulima kilimo cha kisasa chenye mavuno ya uhakika.

Pamoja na hayo amesisitiza Mhandisi Mkazi wa mradi huo, kukaa eneo la mradi hadi pale shughuli za ujenzi zitakapokamilika na thamani ya fedha inayotolewa na serikali ionekane.