December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chongolo amuita Waziri wa Maji Lupeta

Na Zena Mohamed,TimesMajiraOnline,Mpwapwa

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)  Daniel Chongolo amemtaka Waziri wa Maji Jumaa Aweso  kwenda Mpwapwa kabla yeye hajaondoka ilikujibu wananchi kuhusu miradi ya maji ambayo haijakamilika ukiwemo mradi wa maji wa Kijiji cha Lupeta.

Chongolo amesema hayo Wilayani hapa leo Juni 15,2023  wakati alipotembelea katika kijiji hicho ikiwa ni ziara yake ya kutembelea majimbo yote ya Mkoa wa Dodoma,kukagua miradi ya maendeleo ya Mkoa huu ,akizungumza na wananchi wa kijiji hicho  amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa Bilioni 2 kwajili ya mradi wa maji katika kijiji hicho lakini Mkandarasi anahitaji milioni 600 iliakamilishe hajapatiwa.

“Hapa nimeona Mkandarasi anahitaji milioni 600 na kidogo kabla sijaondoka mkoa huu Waziri wa maji atakuja hapa,hizo fedha anakuja nazo au analeta lini,

“Mimi kabla sijaondoka hapa atakuja Waziri na mimi naondoka hapa tarehe 25 na akija hapa aseme mradi unakamilika lini na pesa inakuja lini,hatuwezi kukaa tunasema maneno mengi tunataka matokeo,”amesema Chongolo.

Akijibu maombi ya wananchi kwa chama kuhusu kujengewa Zahanati katika Kijiji cha Lupeta na Bumika   Chongolo amesema atafanyia kazi changamoto ya kutokuwepo kwa zahanati katika vijiji hivyo.

Vilevile Katibu huyo amechangia mifuko 50 ya cement kwaajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya Makutupa iliyoanzishwa ujenzi wake kwa juhudi za Wananchi wenyewe huku akitoa muda wa miezi 9 kukamilishwa kwa ujenzi huo na kuanza kufanya kazi.

Katibu Mkuu Chongolo amehimiza Wazazi kupeleka Watoto mashuleni huku akisistiza kuwa Rais ametoa fedha kwajili ya ujenzi wa chuo cha veta hivyo wakasome 

 “Niwaambie, Elimu sio bure bali ni bila malipo yoyote kutoka kwa wazazi yupo mtu ambaye kaamua kuubeba mzigo wa kulipia ambapo ni Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ndiye anayeoongoza Serikali ya awamu ya sita hivyo Wazazi mnatakiwa kumlipa ukarimu wake kwa kuwapeleka watoto shuleni wakapate haki yao ya kupewa Elimu,”amesema Chongolo.