November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chatanda awataka wanawake kumuenzi Samia kwa kuhudhuria Kongamano

Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online

MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mary Chatanda, amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ambayo haikutarajiwa katika kipindi cha miaka miwili, hivyo wanawake wote, na Watanzania, wamuunge mkono katika jitihada zake za kuleta maendeleoi katika Taifa letu.

Chatanda aliyasema hayo Machi 13, 2023 jijini Dar es Salaam wakati anatoa wito kwa wanawake kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani, kuweza kuhudhuria Kongamano la Kitaifa la miaka miwili ya Rais Dkt. Samia litakalofanyika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam Machi 19, mwaka huu kuanzia saa mbili asubuhi.

Chatanda ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM (CC), alisema kuna mengi ameyafanya Rais Dkt. Samia tangu kuingia madarakani Machi 19, 2021, na kuwaletea heshima wanawake wote Tanzania na duniani kote, hivyo hawana budi kumuunga mkono kwa kila jambo analofanya.

“Ninayo heshima kubwa na taadhima kuwaalika wanawake wote Tanzania Bara na Visiwani. Viongozi wanawake serikalini, viongozi pamoja na wanachama wa vyama vya siasa, tushirikiane katika kumpongeza Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwani ni mwanamke ambaye ametuheshimisha katika utendaji kazi katika kipindi cha miaka miwili, hivyo hatuna budi kumpongeza.

“Wanawake mnaotoka mikoani, tunawaombea mwenyezi Mungu awasafirishe salama mfike salama, hatimaye tuweze kuungana nao katika shughuli hii. Wanawake katika Mkoa wa Dar es Salaam, wao ndiyo wenyeji wa shughuli hii, hivyo waweze kujitokeza kwa wingi katika hafla hii itakayofanyika Uwanja wa Uhuru Machi 19, 2023 kuanzia saa mbili asubuhi… wanawake ni jeshi kubwa, wanawake tunaweza” alisema Chatanda.

Chatanda ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, alisema moja ya mambo ya kujivunia kwa Rais Dkt. Samia ni kuendeleza miradi yote iliyoachwa na mtangulizi wake Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Magufuli ikiwemo Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere, Reli ya kisasa ya SGR na Daraja la Magufuli la Kigongo- Busisi lililopo Mwanza.

“Bado kwenye huduma za kijamii kama afya, elimu, maji, barabara na umeme, kote huko amepeleka fedha, hivyo kuendelea kuwapigania Watanzania kupata huduma, bila kusahau miradi ya maendeleo, ambapo fedha zinapelekwa vijijini ili kutekeleza miradi hiyo” alisema Chatanda.

Mwenyekiti wa UWT Taifa Mary Chatanda (kushoto) akiwa na Mama Anna Abdallah (kulia) ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa UWT Taifa zaidi ya miaka 20 iliyopita.