December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chanjo ya Uviko-19 Shinyanga kufikia zaidi ya watu milioni 1

Na Suleiman Abeid,Timesmajira Online, Shinyanga

MKOA wa Shinyanga unatarajia kuanza zoezi la utoaji chanjo ya ziada ya kujikinga na maambukizi ya Uviko-19 kwa watu wote waliochanja chanjo ya awali pamoja na vijana waliofikia umri wa miaka 18.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme amesema chanjo hiyo itakayofahamika kwa jina “busta” imelenga kuongeza uimara wa kinga kwa waliochanjwa hapo awali na kwamba ni chanjo ileile na siyo mpya.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme akifungua kikao cha tathimini ya chanjo ya kinga ya Uviko-19.

Katika kikao cha tathimini ya chanjo ya kinga ya Uviko-19 mkoani Shinyanga kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa, imeelezwa kuwa mkoa huo umelenga kutoa chanjo hiyo kwa walengwa wapatao 1,071,395 ambao ni wale waliochanja kwenye awamu ya kwanza.

“Walengwa wanaotakiwa kupatiwa chanjo hii ya busta ni 1,071,395 ambao tuliwapatia chanjo za awali, sasa kwa sababu la ongezeko la umri wa vijana wetu inawezekana malengo haya yakaongezeka na kuwafikia watu wengi zaidi ya hawa milioni moja na sabini na moja elfu,”“

Mkuu huyo wa Mkoa ameeleza kuwa zoezi la utoaji wa chanjo ya busta litaanza Juni 16,mwaka huu ili ifikapo Septemba 30, mwaka huu walengwa wote wawe wameishapatiwa chanjo hiyo.

“Nahitaji kupata taarifa za zoezi hili Oktoba mosinmwaka huu ili nione kazi ilivyofanyika,” ameeleza Mndeme.

Ili kuweza kufikia lengo linalokusudiwa Mkuu huyo wa Mkoa amewaagiza wakuu wote wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri katika Mkoa huo kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kwa wananchi wao ili waweze kujitokeza kwa wingi kupatiwa chanjo hiyo.

Amesema Mkoa wa Shinyanga katika awamu ya kwanza ulifanya vizuri kwa kuweza kuvuka lengo ambapo chanjo hiyo ilitolewa kwa asilimia 100.6 na kwamba wananchi wake wana kila sababu ya kujipongeza na waelewe kuwa kinga ni bora zaidi kuliko tiba.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Faustine Mulyutu akitoa taarifa ya hali halisi ya chanjo ya Uviko-19 kwenye kikao cha wadau wa afya mkoani Shinyanga.

Ameeleza kulingana na sensa ya mwaka 2022 kwa sasa wapo wananchi wengi na vijana wanaongezeka kuanzia miaka 18 na kuendelea ambao kwa mwaka huo walikuwa hawajafikia umri huo.

“Sasa ili tuweze kufanikisha zoezi hili lazima tuyashirikishe makundi yote muhimu ya kijamii katika maeneo yetu wakiwemo viongozi wa dini, machifu waliopo mkoani Shinyanga, vyombo vya habari, viongozi wa serikali za vijiji na vitongoji washirikishwe, ili watu wengi waweze kufikiwa,”.

Hata hivyo Mkuu huyo amewataka watendaji wote na wataalamu wa afya wakatoe elimu hiyo kwa kutumia hekima zao badala ya kutumia nguvu na watoe elimu ambayo itawawezesha wananchi kuelewa na waondoe upotoshaji dhidi ya chanjo hiyo ya Uviko-19 inayokwenda kutolewa kwa wananchi.

“Wataalamu wametuambia hapa kwamba bado ugonjwa Uviko-19 sasa kama bado upo, sasa tukapate chanjo, twendeni tukatoe chanjo hii na tumwambie mwananchi chanjo hii ni bure na hakuna gharama yoyote, maana serikali tayari imeishagharimia na tuwaeleze haina madhara kwa mtoto wa kiume wala mtoto wa kike,” ameeleza Mndeme.

Wadau wa afya mkoani Shinyanga wakiwa katika kikao cha tathimini ya Chanjo ya kinga ya Uviko-19.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Faustine Mulyutu amefafanua kuhusu utolewaji wa chanjo hiyo ya busta ambapo amesema mwananchi anapopata chanjo mara nyingi ndivyo anavyoimarisha kinga zake za mwili na kwamba inapotajwa chanjo hiyo siyo kwamba ni chanjo mpya.

“Hii chanjo ya busta siyo mpya ni zilezile ambayo imelenga kuimarisha kinga ya mwili ya mwananchi maana yake ina busti ile ya awali, kwa hiyo tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kwenda kuchanja kama walivyojitokeza mara ya kwanza,”.

Ameeleza kuwa mafanikio yale ya awamu ya kwanza ndiyo yaliwasaidia wakazi wa Mkoa huo wa Shinyanga mbali ya kuvuka lengo lakini waliweza kupunguza vifo pamoja na magonjwa mengine yanayosababishwa na vUviko-19,” ameeleza Dkt. Mulyutu.

Kwa upande wake mmoja wa wataalamu kutoka Shirika la THPS ambaye ni Mkurugenzi wa huduma za kinga kwenye mradi wa afya hatua, Dkt. Appolinary Bukuku amesema shirika lake limeamua kushirikiana na uongozi wa serikali ya Mkoa ili waweze kufikisha ujumbe kwa jamii kupitia viongozi wake.

Wakuu wa Wilaya za Shinyanga, Johari Samizi (kushoto) na Mkuu wa wilaya ya Kahama, Mboni Mhita (kulia) wakifuatilia kikao.

“Sisi THPS ni miongoni mwa wadau wa masuala ya afya hapa nchini na tumeona namna bora ya kushirikisha jamii juu ya hii chanjo ni tuanze na Mkuu wa Mkoa, tumemwalika hapa amekuja ameongea na Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi ambao wao ndiyo wenye watu huko chini,” amesema na kuongeza kuwa

“Kadri maagizo yanayotolewa na Mkuu wa Mkoa ni wazi yatashuka chini kupitia Wakuu wa Wilaya kwenda kwa viongozi wa kata, vijiji na vitongoji kama alivyoagiza hapa maana wao ndiyo wenye watu na wataweza kufikisha ujumbe hadi ngazi ya chini, sisi kazi yetu ni kutoa elimu kwa jamii,”.