March 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Changamoto za mabadiliko ya tabianchi zinavyoweza kuathiri ustawi wa familia,watoto

Judith Ferdinand

Mabadiliko ya tabianchi yamekuwa na athari kwa familia na watoto mkoani Mwanza, huku changamoto za kiuchumi zikionekana kuathiri moja kwa moja ustawi wa familia na maendeleo ya watoto

Hata hivyo, juhudi za Serikali na jamii bado zinaendelea ili kukabiliana na hali hii ya mabadiliko ya tabianchi na kutafuta suluhu zinazoweza kusaidia watoto na familia zao kuendelea na maisha bora.

Wakati wazazi wanakumbwa na changamoto za kiuchumi kutokana na mabadiliko ya tabianchi, watoto wanasema kuwa wanashuhudia kupungua kwa huduma muhimu kama elimu, chakula, na afya. Watoto hao wamesema kuwa ni wao walioathirika moja kwa moja pale wazazi wanaposhindwa kuhimili changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Ofisa mradi wa ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi kwa watoto Mkoa wa Mwanza kutoka MYCN Zakia Selemani,akitoa elimu ya mabadiliko ya tabianchi kwa baadhi ya wanafunzi.

Katika mahojiano na Timesmajira Online, baadhi ya watoto mkoani Mwanza, wakiwemo wanafunzi wa shule ya msingi Magaka na wanahabari watoto wa shirika la Mtandao wa Watoto na Vijana Mwanza (MYCN), wamesema kuwa mabadiliko ya tabianchi,yanasababisha kuwa na mvua nyingi kupita kiasi na kuleta mafuriko, ukame, au jua kali kupita kiasi, yanaathiri shughuli za kiuchumi zinazotegemea kilimo, ufugaji, na uvuvi.Hali hii inafanya familia nyingi kupungukiwa na mapato, na hivyo watoto kutopata huduma muhimu za kila siku.

Samweli Fides, mwanafunzi wa shule ya msingi Magaka wilayani Ilemela, anasema kwamba familia zinazotegemea kilimo, ufugaji, au uvuvi huthubutu kupungukiwa na mapato pindi inapotokea mafuriko au ukame. “Mafuriko na ukame husababisha mazao kunyauka au kusombwa na maji, na hivyo uchumi wa familia kushuka,” anasema Fides. “Hali hii inamaanisha kuwa watoto wanakosa huduma za msingi kama chakula na elimu. Ikiwa familia ilizoea kutoa milo mitatu kwa siku, huenda watoto wakala mlo mmoja au miwili tu,”.

Brightness Boniface,mwanahabari mtoto kutoka MYCN, anasema kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi zinaathiri watoto moja kwa moja. “Wazazi wanaposhindwa kutimiza mahitaji ya msingi, watoto wanakosa haki yao ya kupata elimu, matibabu, na chakula cha kutosha,” anasema Boniface. “Mfano mzuri ni pale mzazi anaposhindwa kuendeleza shughuli za kilimo kutokana na mafuriko au ukame, ambapo mavuno huwa kidogo au hayapatikani kabisa.”

Ofisa Mazingira wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, David Mgunda, anakubaliana na watoto hawa nakusema kwamba jamii ya Mwanza inategemea kilimo na ufugaji, na mabadiliko ya tabianchi yanaathiri sana sekta hizi.

“Hali ya ukame husababisha mifugo kukosa malisho, na mazao kunyauka. Kwa upande mwingine, mvua zinaposhindwa kunyesha kwa wakati unaofaa, mavuno huwa duni na familia zinakosa kipato cha kutosha,” anasema Mgunda.

Mgunda pia anaongeza kuwa athari za ukame na mabadiliko ya tabianchi pia zinahusisha matatizo ya maji. “Visima vinavyotumika katika maeneo ya vijijini hujaa maji kidogo au kutoweka kabisa, na familia zinaishia kutumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya shughuli za kiuchumi,” anasema na kuongeza:

“Hali hii pia inachangia kupungua kwa mahudhurio ya wanafunzi shuleni, kwani watoto wanaungana na familia kutafuta maji.”

Anasema,mabadiliko ya tabianchi pia inachangia kuongezeka kwa magonjwa kutokana na joto kali na mafuriko, ambapo familia hutumia kipato chao kwa matibabu. “Watoto wanakosa fursa ya kupata elimu bora kutokana na fedha kupungua ambazo zingesaidia kununua mahitaji muhimu ya shule, hali inayosababisha kiwango cha elimu kushuka na kuathiri maendeleo yao,” anasema Mgunda.

Ofisa Mradi wa ustahimilivu endelevu wa mabadiliko ya tabianchi kwa watoto mkoani Mwanza kutoka MYCN Zakia Selemani,anasema,kupitia mradi huo wamefanikiwa kufanya tathimini fupi ya athari za mabadiliko ya tabianchi kwa watoto katika Wilaya ya Ilemela na Nyamagana

“Tulichobaini jamii bado haina uelewa juu ya mabadiliko ya tabianchi,yanasababishwa na nini,pia jamii haimtazami mtoto kama muathirika wa mabadiliko ya tabianchi,hivyo wanaamini mabadiliko hayo yanamuathiri mtu mzima tu,lakini mtoto anatirika moja kwa moja na mabadiliko hayo,”anasema Zakia.

Zakia anasema,katika tathimini hiyo kwa upande wa Wilaya ya Ilemela kwenye jamii za uvuvi ambao uchumi wao kwa asilimia kubwa unategemea shughuli hiyo,jua linapotokea kuwa kali kupita kiasi husababisha maji ziwani kupungua na mazao ya samaki nayo huama.

Kama wazazi wote wanafanya shughuli za uvuvi inawalazimu kusafiri kwenda visiwani au maeneo ya mbali kutafuta mazao ya uvuvi ikiwemo dagaa na samaki,hivyo kuwaacha watoto wakiwa pekee yao,hali hiyo inaathiri moja kwa moja watoto kwenye malezi ambao wanahitaji malezi ya mtu mzima wa kusimamia maadili na upatikanaji wa mahitaji muhimu kama vyakula.

“Unakuta mzazi anasafiri kwa miezi miwili mpaka mitatu anafanya kuwasiliana na watoto kwa simu na kutuma matumizi,kunakuwa hakuna mtu wa kumfuatilia mara kwa mara kuhusu maendeleo na mahudhurio yake shuleni,mfano Ilemela kuna shule moja mwanafunzi mmoja wakati yupo darasa la sita mwaka jana alimaliza miezi kadhaa bila kuhudhuria masomo na badala yake alienda wakati wa mtihani,alivyofika darasa la saba mzazi aliulizwa kwanini mtoto wakoa anamaliza miezi mingi bila kuhudhuria shuleni,akajibu alikuwa visiwani hii inaonesha watoto wanajilea wenyewe jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wao na kinyume na sheria ya mtoto ya mwaka 2009,”anasema Zakia.

Pia anasema,kupitia tathimini hiyo walibaini changamoto nyingine inayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi na kuathiri watoto ni huapatikanaji maji kuwa wa shida.

Anasema,kutokana na tamaduni za jamii za kitanzania mtoto kazi yake ni kuhakikisha anatafuta maji kwa ajili ya matumizi ya familia,hivyo inapotokea ukame au jua kuwa kali zaidi kunakuwa na upungufu wa maji,huku akitolea mfano watoto wa Kisiri waliwaeleza kuwa,kutokana na hali hiyo wanalazimika kufuata maji saa kumi usiku kabla ya kwenda shule.

Nakutokana na foleni ya kuchota maji kuwa kubwa wanarejea nyumbani saa 11,alfajili kwa ajili ya kujiandaa kwenda shuleni hali hiyo inaweza kuathiri ustawi wa elimu.

“Wakati wa kiangazi hupatikanaji wa maji shuleni unakuwa changamoto, hivyo wanakosa ya maji ya kujisafisha wakati wa kujisaidia haja na kwa upande wa watoto wa kike inakuwa changamoto akipata hedhi wakati yupo shuleni sanjari na maji safi ya kunywa,”.

Sanjari na hayo Zakia,anasema,mabadiliko ya tabianchi yaathiri kilimo na mojo kwa moja athari zake zinaikumba jamii wakiwemo watoto,huku akitolea mfano jamii ya kisukuma inategemea shughuli za kilimo katika uchumi.

Hivyo inapotokea kuwa na kiangazi kwa muda mrefu,jua kuwa kali kupita kiasi au mvua kuwa nyingi kupita kiasi kama kipindi cha nyuma,mazao yanaharibika,hali hiyo inaweza kusababisha familia kupata mazao kidogo au isipate kabisa na kuchangia kipato cha wazazi kushuka kwani wanategemea mazao hayo kwa ajili kuuza na mengine yatumike kama chakula.

“Wazazi wanapokosa fedha za kutosha za kuhudumia familia moja kwa moja waathirika wakuu wa hali hiyo ni watoto kwani watakosa kuhudhuria vyema shuleni kwa kukosa mahitaji muhimu kama vile daftari, kwa sababu mzazi anaweza kushindwa kugawanyisha kipato hicho kidogo kutimiza mahitaji yote ya familia,pia upungufu wa chakula utasababisha njaa hivyo kuchochea ushiriki duni wakati wa kujifunza darasani na uelewa duni wa kili kinachofundishwa sanjari na kusababisha utapia mlo,”anasema Zakia.

Zipi jitihada za Serikali,wadau kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

Ofisa Mazingira wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, David Mgunda,anasema licha ya changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, Mgunda,Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali kukabiliana na mabadiliko hayo.

“Serikali imeweka sheria mbili muhimu za usimamizi wa mazingira, ambazo ni Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na sheria ndogo za Halmashauri.Sheria hizi zinazuia uharibifu wa mazingira, kama vile ukataji miti holela na uchafuzi wa vyanzo vya maji, ili kulinda mazingira kwa manufaa ya jamii,”.

Ofisa Mradi wa ustahimilivu endelevu wa mabadiliko ya tabianchi kwa watoto mkoani Mwanza kutoka MYCN Zakia Selemani,anasema kupitia mradi huo,wanahakikisha mtoto anakuwa sehemu ya mapambano ya mabadiliko ya tabianchi kwa kupata fursa ya kushirikishwa moja kwa moja,Pia wanaendlea kutoa elimu kwa jamii ili kuwajengea uelewa juu ya mabadiliko ya tabianchi,nini kina sababisha,atahari zake zipoje na namna gani ya kukabiliana nayo.

Pia wamekuwa wakifanya midahalo katika shule mbalimbali zilizopo kwenye kata ambazo mradi unafanya kazi katika Wilaya ya Ilemela na Nyamagana wakitumia wanahabari watoto wa shirika hilo,mabaraza ya watoto ya wilaya hizo,wanafunzi pamoja na kupanda miti katika maeneo ya shule hizo.

Hata hivyo serikali haijakaa kimya katika jambo hili ambapo ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi imekuwa ikihamasisha upandaji wa miti ili kuweza kurejesha uoto wa asili ambayo ndiyo njia kuu ya kupambana na mabadiliko hayo,huku ikizindua mpango mkakati wa miaka 10(2024-2034),matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza ukataji miti kwa ajili ya nishati ya kupikia.

Lengo la mkakati huo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2034,asilimia 80 ya watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.