January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chande:Mapambano dhidi  ya magendo ni jukumu letu sote

*Amezindua boti ya doria yenye thamani ya milioni 530

*TRA yawataka wananchi waone magendo ni adui

Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Mwanza

Serikali imesema, biashara ya magendo ni vita kubwa nchini,hapa ambayo inachangia  kukosesha  taifa mapato,kuathiri afya za wananchi pamoja na kuharibu mazingira.Hivyo jukumu la kupambana na vita hiyo ni la kila mtu.

Katika kukabiliana na vita hiyo,Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA),imezindua boti yenye thamani ya milioni 530, ya kufanya doria ndani ya Ziwa Victoria,ili kudhibiti uingizwaji wa bidhaa kwa  magendo,ambazo kwa kiasi kikubwa hupitishwa kwa njia ya maji.

Hayo yamebainishwa mkoani Mwanza Desemba 12,2024,,Naibu Waziri wa Fedha Hamad Chande,wakati wa hafla ya uzinduzi wa boti ya doria ya TRA,itakayofanya kazi ndani ya Ziwa Victoria,ambapo amesema zinahitajika nguvu za pamoja  katika kupambana na magendo ambayo yanaonekana hasa katika njia za majini  kwa sababu  ya uwepo wa bandari bubu nyingi.

Pia amesema kuna milango mingi ya kutoka Mkoa hadi Mkoa,au Mkoa na Kisiwa ama kutoka nchi hadi nchi ambayo inatumika kupitisha bidhaa za magendo kwa njia ya maji,hivyo rai waunge mkono kazi inayofanywa na TRA.

“Nitoe wito kwa wananchi wenzangu wawe tayari kupambana na magendo kwa njia yoyote na nguvu yoyote ambayo Mungu amewajalia.Tufike mahali katika sifa tatu,tuwe nayo moja,ukiona mtu anapitisha au anafanya magendo  toa taarifa kwa ulimi wako na uliseme jambo hilo,”amesema Chande na kuongeza:

“Pili ukishindwa kulisema,basi ondoa ili zoezi lisifanyike na hilo likishindikana basi chukia kwamba tendo hili ni ovu.Kwa bahati mbaya leo baadhi ya watu wanafurahia na kuona ili mtu aonekane mjanja na jasiri ni yule anaye kwepa kodi au kufanya biashara haramu ya magendo na jamii inashindwa hata kumchukia mtu huyo,”.

Sanjari na hayo,amewataka wafanyabiashara wote nchini kulipa kodi kwa hiari bila shuruti ili kuchochea maendeleo yao binafsi na taifa pamoja na kuepuka kutozwa faini na hata kufungiwa akaunti.

Hata hivyo amesema,boti hiyo  itasaidia  katika harakati za kupambana na vita ya magendo nchini hapa,hivyo ametoa wito kwa taasisi zote ambazo zinahusika kushirikiana na TRA, kudhibiti biashara ya magendo,kulinda uchumi  na usalama wa taifa,afya za wananchi na mazingira.

Kamishina Mkuu wa TRA,Yusuph Mwenda,amewataka wananchi wawaone wanaofanya magendo ni adui wasioitakia mema nchi,kwani  zinaathiri uchumi na kuhujumu biashara nyingine.

Pia amesema biashara hizo ,zinaathiri  afya za wananchi kwani moja ya bidhaa za magendo zinazopita Mkoa wa Mwanza kutoka nchi jirani  ni vipodozi,ambavyo kabla havijaingia nchini lazima vikaguliwe  na TBS na TMDA.Hivyo  vikiputishwa kwa magendo vinaweza kuingizwa ambavyo ambavyo havistahili na kuhatarisha afya za wananchi sanjari na kuchochea rushwa.

“Wakati TRA inaanzishwa tulikuwa tunakusanya bilioni 42 wastani kwa mwezi,lakini kwa sasa tunakusanya wastani wa tirioni 2.5, kwa mwezi,ni mafanikio makubwa yaliotokana na wananchi kulipa kodi kwa hiari inavyostahili,”.

Kwa upande wake,Kamishina wa Forodha wa TRA,Juma Hassan,amesema mwaka 2021/2022  Serikali kuidhinisha bajeti ya zaidi ya  bilioni 2 kwa ajili ya TRA kununua boti nne za kufanyika doria ikiwa ni njia ya kudhibiti biashara ya magendo,kati ya hizo tatu ni za wazi huku moja ni ya kufunikwa.

“Boti moja ya kufungwa ina thamani ya milioni 865.1, ambayo ujenzi wake unaendeleaje huku boti tatu za wazi ikiwemo iliozinduliwa Mwanza zinathamani ya bilioni 1.6 ambapo kila boti inathamani ya milioni 530.Ambapo boti mbili zilipokelewa Aprili 2023 boti mbili moja tuliipeleka Dar-es-Salaam  na nyingine  Tanga kwa ajili ya kufanya doria katika Bahari ya Hindi  na iliozinduliwa leo(jana) jijini Mwanza itafanya kazi ndani ya Ziwa Victoria,”amesema Juma.

Hata hivyo amesema,katika kukabiliana na changamoto ya magendo mwaka 2022/2023, TRA kwa kushirikiana na vyombo vingine mbalimbali walifanikiwa kukamata bidhaa za magendo zenye thamani ya bilioni 46.26 sawa na ongezeko la asilimia 124.56, ikilinganishwa na magendo yaliokamatwa  kwa kipindi kama hicho mwaka 2021/2022.

Ambapo mizigo iliokamatwa baadhi ililipishwa kodi na adhabu stahiki na kukabidhiwa kwa wenyewe,baadhi ya mizigo ilitaifishwa na kuuzwa, mingine iligawiwa kwenye taasisi zenye uhitaji na baadhi iliokuwa haifai kwa matumizi ya binadamu ziliteketezwa.

Amesema,katika kipindi cha mwaka 2023/2024, bidhaa zilizoteketezwa zilikuwa na thamani ya bilioni 1.01,ongezeko la asilimia 120.6 ya bidhaa zilizoteketezwa mwaka 2022/2023.

Katika kipindi cha 2023/2024 bidhaa zilizotsifishwa na kugawiwa kwa wahitaji zilikuwa na thamani ya milioni 297.5, ambayo ilikuwa pungufu ya asilimia 39.7, ya thamani ya bidhaa iliogawiwa kwa wahitaji mwaka wa 2022/2023.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi, amesema Mkoa wa Mwanza  utashirikiana na TRA, kuhakikisha malengo ya boti hiyo yanafikiwa kwa kukusanya mapato  na kuongeza pato ya taifa.

Makilagi,ametaja faida ambayo Mkoa wa Mwanza umepata  kwa kuchangia Pato la taifa kwa kushika nafasi ya pili umepatiwa  zaidi ya tirioni 5.7, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali mkoani hapa.