Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online, Shinyanga
BAADHI ya wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Shinyanga (SHIRECU) wameelezea kushitushwa kwao na kampeni inayoendelea hivi sasa ya kuvishinikiza baadhi ya vyama vya Ushirika vya msingi (AMCOS) kujitoa katika chama hicho.
Hali hiyo imeelezwa huenda ikasababisha kusambaratika kwa Chama hicho kikuu cha ushirika mkoani Shinyanga ambacho ni miongoni mwa vyama vikuu vikongwe vya ushirika hapa nchini ikiwemo vile vya KCU (Kagera), NCU (Mwanza) na KNCU (Kilimanjaro).
Wakizungumza na mwandishi wa Timesmajira Online siku chache baada ya kufanyika kwa mkutano mkuu wa 28 wa SHIRECU wanachama hao wamesema kampeni inayoendelea hivi sasa ni ya kuvishinikiza vyama vya ushirika vya msingi vilivyoko wilayani Kishapu vijitenge na SHIRECU na viunde ushirika wa Kishapu.
Wamesema shinikizo hilo linachangiwa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya viongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM wilayani Kishapu, Shija Ntelezu na waliokuwa viongozi ndani ya SHIRECU vipindi vya nyuma.
Inasemekana mpaka hivi sasa zaidi ya vyama vya msingi vya Ushirika (AMCOS) 46 tayari vimeandika barua vikiomba kujitoa SHIRECU na kuunda Chama Kikuu kingine kipya cha Ushirika cha wilaya ya Kishapu.
Hata hivyo agenda ya kutaka kujitoa SHIRECU iliyotakiwa kuingizwa kwenye agenda za mkutano mkuu wa 28 wa SHIRECU ilikwama baada ya kubainika barua iliyoandikwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu inazungumzia kuundwa kwa Chama kipya cha Ushirika ambayo ni kazi ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini na siyo mkutano mkuu wa SHIRECU.
“Kwa kweli ni jambo la kusikitisha kuona viongozi wetu ambao ndiyo wanaopaswa kushirikiana kukiimarisha Chama chetu Kikuu cha Ushirika ndiyo wako mstari wa mbele kuona SHIRECU inasambaratika, na yote hii undani wake ni uwaaniaji wa madaraka ndani ya chama kipya kitakachoanzishwa,”
“Hali ya SHIRECU kwa hivi sasa inaridhisha kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na ilivyokuwa miaka ya nyuma chini ya uongozi wa waliokuwa viongozi wa chama hiki ambao ndiyo wamesimama kidete kuona Amcos za Kishapu zinajitenga na kuunda ushirika wao, hapana hili lisiruhusiwe,” anaeleza Justine Lugega.
Lugega anafafanua kuwa pamoja na agenda ya kujitoa kukwama ndani ya mkutano mkuu wa SHIRECU ambao umefanyika mwishoni mwa wiki iliyopita hivi sasa vigogo hao akiwemo mwenyekiti wa CCM wanaunda timu ya baadhi ya watu kwenda Dodoma kukutana na waziri wa kilimo, Hussein Bashe.
“Sisi tunamuomba waziri Bashe awe makini, asikurupuke kutaka kuwakubalia watu hawa, ikibidi awahoji kwanza na kwa kina kwa nini wanataka kujitoa SHIRECU, kama ni suala la uongozi mbovu, zipo taratibu za kuwaondoa madarakani viongozi wasiotimiza wajibu wao, dawa siyo kujitenga,”
“Hali ya SHIRECU kwa sasa ni nzuri sana ikilinganishwa na miaka saba iliyopita huko nyuma, sasa badala ya watu tuunganishe nguvu ili SHIRECU iendelee kuimarika leo watu wanataka kuisambaratisha, hapana, Bashe arejee Ilani yao ya Uchaguzi ya CCM, inaeleza nini kuhusu Ushirika hapa nchini,” anaeleza Lugega.
Kwa upande wake mwanachama mwingine, Charles Shigino pamoja na kukiri kuwepo kwa mipango ya kutaka vyama vya Amcos Kanda ya Kishapu kutaka kujitoa hata hivyo anasema ni vyema badala ya kujitoa pawepo na utaratibu wa kuangalia kwa nini SHIRECU imekuwa ikisuasua kwa kipindi kirefu.
“Ni kweli hata mimi ni miongoni mwa watu tuliokuwa tunaunga mkono kujitenga na kutaka kiundwe Chama Kikuu kipya cha Ushirika cha Wilaya ya Kishapu kama ilivyofanyika kwa watu wa Kahama ambao waliunda chama chao Kikuu cha Ushirika cha wilaya ya Kahama (KACU),”
“Lakini naona kujitoa ama kuunda chama kipya siyo ufumbuzi wa tatizo, kikubwa ni vyema kuketi na tuangalie tatizo lipo wapi linalosababisha kusuasua kwa Ushirika wetu, kama ni ubovu wa Bodi au Menejimenti basi wahusika waondolewe madarakani tuweke viongozi wenye sifa, ushirika uendelee,” anaeleza Shigino.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, Shija Ntelezu amekiri kuwepo kwa mpango wa baadhi ya vyama vya msingi (AMCOS) wilayani Kishapu kutaka kujitoa SHIRECU na kuunda chama kipya cha Ushirika cha wilaya ya Kishapu.
Hata hivyo amekanusha madai ya kwamba yeye ni miongoni mwa watu wanaoshinikiza kugawanyika kwa wanachama wa SHIRECU na kumtaka mwandishi aeleze kuwa wana Kishapu ndiyo wanaotaka kuunda Chama chao cha Ushirika cha Kishapu.
“Mimi sishinikizi kuvunjwa kwa SHIRECU wewe andika kwamba wana Kishapu wameazimia kupata Union yao ya Kishapu kama walivyopata KACU na Mbogwe, sasa ninyi mkisema tunavunja mnapotosha, sisi tunataka chama chetu kwa ajili ya maendeleo ya watu wa Kishapu,”
“SHIRECU haina changamoto kubwa, wanaotaka kubaki SHIRECU wabaki huko, wale wanaounga mkono kuundwa kwa Chama kipya tutakuwa nao, na sisi Kishapu sasa tumekuwa tuna uwezo wa kujiendesha, tunataka tuwe na Jineri yetu wenyewe huku, tunakusanya mapato mengi kwa mwaka, na tutaweza kukopesheka,” anaeleza Ntelezu.
Kuhusu suala la kuundwa kwa timu ya watu kwenda kuonana na waziri Bashe, mwenyekiti huyo amekiri na amesema tayari wako mbioni kwenda Dodoma ili kukutana na waziri aweze kubariki kuundwa kwa ushirika mpya wa Kishapu.
“Usitake kujua timu hiyo itagharamiwa na nani, hata ikibidi kutembea kwa miguu kwenda Dodoma tutatembea ili mradi tu tuweze kukutana na Waziri Bashe, hili lina baraka zote za Chama cha Mapinduzi, Madiwani na mbunge wetu tumekubaliana, sasa kwa nini mnatuonea nongwa?” anahoji Ntelezu.
Akishiriki katika mkutano mkuu wa 28 wa SHIRECU mbunge wa Jimbo la Kishapu, Boniface Butondo alisema suala la watu kujitenga halina mjadala bali kikubwa kinachotakiwa ni watu kufuata utaratibu kwa kuzingatia sheria na kanuni za ushirika zilizopo badala ya watu kuzuiwa kutekeleza adhima yao.
“Ninachotaka niseme ni kwamba habari imeishafika kuwa vyama 57 vya Kishapu vinataka kujiondoa na kuanzisha Chama Kikuu cha kwao, sheria iko wazi inaruhusu, taratibu zinazofuata ni ambazo mkutano mkuu utatambua juu ya haya, lakini wale wanaojiondoa watapaswa kuzifuata tu zile tararibu ya namna ya kuondoka,” anaeleza Butondo.
Kaimu Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoani Shinyanga, Deogratias Momburi akichangia hoja kwenye mkutano mkuu wa 28 ameshauri suala hilo iwapo lipo ni vyema likazingatia sheria za ushirika zilizopo badala ya kulitekeleza kienyeji.
“Kama kuna watu wanataka kujitoa SHIRECU vipo vifungu vya sheria vinavyoelezea ni njia zipi za kufuata ili mtu kujitoa, lakini pia hata masharti yenu ya Chama yameeleza ni jinsi gani mwanachama anaweza kujiunga ama kujitoa ndani ya chama,”
“Sasa kwenye barua yenu hii nimeangalia hakuna neno la kujitoa bali kuna kusudio la kutaka kuunda chama, hili la kuunda Ushirika mpya hapa siyo mahala pake sasa lazima mzingatie kile kinachoelezwa ndani ya kanuni ya 78 na kifungu cha 58, ili suala hili liweze kujadiliwa muwe na hoja ya kutaka kujitoa SHIRECU,” anaeleza Momburi.
Miongoni mwa sababu za kujitoa SHIRECU zinazotajwa na hivyo ni pamoja na Chama hicho Kikuu kuzidiwa na madeni na ikidaiwa hivi kwa sasa kimeshindwa kujiendesha kwa faida hali inayochangia kisiweze kukopesheka na Taasisi mbalimbali za kifedha hapa nchini.
Katika taarifa yake kwenye mkutano mkuu wa 28 wa SHIRECU mwenyekiti wa Chama hicho Kwiyolecha Nkilijiwa amesema katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 SHIRECU imefanikiwa kukusanya mapato kutoka vyanzo vyake mbalimbali vya mapato kiasi cha shilingi 1,126,456,332.00.
Pia chama hicho kimeingia mkataba na Chuo cha Serikali za Mitaa nchini wa kupangisha sehemu ya jengo lake la Makao Makuu kwa malipo ya kodi ya shilingi milioni 95 kwa kila mwaka hali inayotajwa itawezesha mapato ya chama hicho kuongezeka zaidi.
More Stories
Mussa: Natamani kuendelea na masomo,nikipata shule ya bweni
Tanzania inavyowahitaji viongozi wanawake aina ya Mwakagenda kuharakisha maendeleo
SCF inavyotambua jitihada za RaisSamia mapambano dhidi ya saratani