November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chama cha wauguzi chalia na muundo wa watumishi ngazi ya mshahara

Na George Mwigulu, Timesmajira Online,Katavi

Serikali imeombwa kushughulikia muundo wa utumishi ngazi za mshahara kwa kuwa tatizo hilo limedumu kwa muda wa miaka 13 pamoja na muundo wa utawala ambao kwa kiasi kikubwa unadhorotesha weledi wa utendaji kazi wa watumishi wa afya hususani wauguzi na wakunga.

Rais wa Chama Cha Wauguzi Tanzania, Alexander Balubya (katikati) akiwa na Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Katavi,Juma Masasi (Kushoto) na Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Katavi,Medard Nguma wakati wa mkutano mkuu.

Rais wa Chama Cha Waunguzi Tanzania (TANNA), Alexander Balubya akizungumza Februari 3,2024 katika ukumbi wa Polisi Klabu Manispaa ya Mpanda wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho Mkoa wa Katavi ameeleza maombi hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maadhimio ya mkutano mkuu yaliyofanyika Mei 12,2023 jijini Mwanza.

Balubya amefafanua kuwa wauguzi walishatoa mapendekezo kwa mamlaka husika lakini hadi sasa hakuna utekelezaji wowote wa muundo wa utumishi ngazi ya mshahara uliofanyika licha ya kuwa wasikivu na wazalendo lakini serikali ni kama haioni umuhimu wao huku siku hadi siku utoaji wa huduma za afya ukidhorota.

“Serikali inajenga vituo vingi sana vya afya lakini kama hapatakuwa na uwekezaji na kutambua wataalamu hawa bado jitihada zao hazitakuwa na tija kwa maana wataalamu hawa ni uti wa mgogo kwenye huduma za afya kwani muda wote utakutana na muuguzi na mkunga…naiomba serikali isifumbe macho,” amesema.

Pia wameiomba serikali kufanya marejeo ya muundo wa utawala hususani kupitia wizara ya OR-TAMISEMI kwa kuwa kuna mabadiliko mengi yamefanyika yanaenda kumuondolea nafasi ya usimamizi muuguzi na mkunga kwenye maeneo yake ya kazi.

“Tunaomba wafanye marejeo wawarudishe kwenye utawala wa usimamizi kwa sababu pasipokuwa na usimamizi kwenye huduma za wauguzi na ukunga utaathiri mfumo mzima wa utoaji wa huduma za afya,”

Rais huyo wa TANNA amebaini kero ya wauguzi kwa baadhi ya halmashauri za Mkoa wa Katavi kushindwa kutoa posho za sare na kuwa mjadala wa muda mrefu kwani hapo awali serikali ilitoa kutoka hazina kuu lakini baada ya kupeleka madaraka chini maana yake kila kituo husika kinapaswa kuwa na mpango madhubuti wa utoaji wa posho za sare.

Licha ya kazi nzuri ya serikali ya Mkoa wa Katavi katika kushughulikia kero za watumishi ameiomba kupitia Katibu Tawala kuzielekeza mamlaka za halmashauri anazoziongoza kuendelea kutekeleza takwa hilo la kisheria ambapo wauguzi wanatakiwa kupata sitahiki zao posho za sare na masaa ya ziada kazini.

Amesema serikali ina mamlaka ya kuhakikisha inatengeneza mazingira rafiki na wezeshi kwa wataaluma kutimiza wajibu wao wa kutoa huduma zilizo safi na salama na rafiki kwa wateja.

Mwenyekiti wa Chama cha Wauguzi Mkoa wa Katavi,Juma Masasi amesema kuwa lengo la mkutano mkuu huo ni kukutana pamoja na kujadili masuala ya mktadha kuhusu wataaluma na kuweza kuelimishana ushiriki hai wa shughuli nzima za chama hicho nchini.

Aidha amesema kuwa kikao hicho kimelenga kutoa taarifa kwa wananchama maadhimio ya mkutano mkuu uliofanyika mwaka jana jijini Mwanza.

Baadhi ya wauguzi wa Mkoa wa Katavi wakiwa katika ukumbi wa Polisi Club Manispaa ya Mpanda kwa ajili ya mkutano mkuu wa chama cha wauguzi wa mkoa huo

Muuguzi Mkuu wa Manispaa ya Mpanda,Victoria Mtitu amesema kwamba licha ya kuwa na kero mbalimbali ambazo hazijatatuliwa na zingine zikiendelea kutatuliwa wanaowajibu wa kufanya kazi kwa bidii kwa maslahi ya watu.

Victoria ameeleza kuwa kuna baadhi ya mambo wamekuwa wakilaumiwa ya kimaadili kutokana na kushindwa kutimiza wajibu wa kazi jambo ambalo kama hawatayashughulikia wanataaluma imani na dhamana waliyopewa itapungua kwa wananchi.

August Thomas,Ofisa Muuguzi Msaidizi wa Manispaa ya Mpanda ameshauri viongozi wa chama hicho Wilaya ya Mpanda na Mkoa kuwaalika makatibu afya kwenye vikao vya ndani kwa sababu wanafahamu namna ya kugawa vifungu vya fedha.

Rais wa Chama Cha Wauguzi Tanzania, Alexander Balubya akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa Chama hicho Mkoa wa Katavi