January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chalamila: Hongereni mliofungua maduka Kkoo, mliofunga nitawalindia maduka yenu

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Dar

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amefikia katika Soko la Kariakoo, leo Juni 24, 2024, kufuatilia mgomo wa wafanyabiashara unaoendelea, ambapo amewapongeza wanaoendelea kufanya biashara na kuahidi kuyalinda maduka ya waliofunga kwa mgomo.

Akizungumza na baadhi ya wafanyabiashara katika Soko hilo, mbele ya Waandishi wa Habari, Chalamila amesema “nimeona nipite kuhakiki kile kinachoongelewa, nawapa hongera wale wote mliokubali kufungua maduka hapa Kariakoo, asanteni sana na nyinyi mnaoendelea kufunga nawathibitishia kuwa nitazilinda biashara zenu wala hakuna mwizi atakayeiba, hivyo taka mkitaka kufunga kwa mwezi sawa wakati sisi tukiendelea kushughulikia yale yote mliyopeleka Serikalini.

Biashara siyo siasa, leo hii hii jioni mtaona kuna hasara imeingia, wala hutakiwi kusubiri kesho wala kesho kutwa kwani siasa huwezi kugundua hasara zake”, amesema Chalamila.

Pia Chalamila, amewataka wafanyabiashara hao kutumia uhungwana kabla ya kufanya maamuzi yasiyo sahihi, huku akisema kuwa, Serikali ipo kwa ajili ya kulinda maslahi ya wananchi wake ikiwa pamoja na wafanyabiashara.

“Nikisema mimi Mkuu wa Mkoa nije dukani kwako kuangalia kiwango kikubwa cha ukwepaji kodi unaofanyika nyie mtaishi hapa? Siyo kuwa Mimi ni chizi na siyo kwamba sina akili, nafahamu kwamba kuna wakati mwingine risiti hamtoi, sijawahi kuwapeleka Mahakamani lakini nyie ndani ya muda mfupi tu tayari maduka mmefunga, basi sawa Mungu atatufikisha mahali pema”, amesema Chalamila.

Aidha, amewaondoa hofu wafanyabiashara waliofungua biashara zao kuwa, waendelee kufanya biashara zao kwa amani na hakuna atakaye wasumbua “niwaondoe hofu wale wote mliofungua maduka yenu kuwa, hongereni na hakuna mtu yoyote atakayewasumbua, pia yale yote mliyopeleka sehemu husika kama ni Bungeni yanaendelea kushughulikiwa, lakini niwaulize ndugu zangu, ikitokea mambo haya yanachukua hata muda wa mwezi mmoja na mimi niseme Askari wangu walinde eneo hili na hakuna mtu kufungua duka mpaka tutakapo suluhisha kwa mwezi mzima itakuwa sawa au siyo sawa?”, aliuliza Chalamila.