February 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jamii yatakiwa kutafsiri maendeleo yanayofanywa na Rais

Na Mwandishi wetu Timesmajira online

MKUU wa Mkoa wa Dar es salaam Albert Chalamila amewataka viongozi na wataalamu Mkoani humo kutafsiri vema na kwa vitendo maendeleo yanayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya elimu na afya ili iwe na tija kwa jamii hususani katika kuinua ufaulu wa wanafunzi kwenye shule ambazo hazifanyi vizuri.

Chalamila ameyasema hayo Jijini Dar es Wilayani Temeke leo Februari 10,2025 katika mkutano na wadau mbalimbali wa elimu amesema Serikali chini ya Rais Dkt Samia imekuwa ikiimarisha miundombinu ya elimu na mazingira ya kufundishia na kujifunzia hivyo ni muhimu kwa kila mdau wa elimu ikiwemo wazazi, viongozi pamoja wataalamu kujielekeza kwenye kusaidia watoto ili kuinua viwango vya ufaulu kwa wanafunzi

Amesema kuwa badala ya kutazama sababu chache zinazotolewa na kuonekana kusababisha ufaulu kuwa hafifu ni muhimu kufanya utafiti wa kina na kuhakikisha wazazi wanashirikishwa ipasavyo kwenye kuinua ufaulu wa wanafunzi ili ndoto za Rais Dkt Samia zitimie na fedha nyingi anazozitoa kuimarisha miundombinu ya elimu zitimize lengo husika.

Vilevile Chalamila amesema hivi karibuni Serikali Mkoani humo inatarajia kufanya mkutano utakaojumuisha wazazi na wadau wengine wa elimu ili kujadili kwa pamoja na kuimarisha ushirikishwaji wa wazazi kwenye masuala ya elimu.

Naye Mkuu wa wilaya ya Temeke Sixtus Mapunda amesema wanakwenda kujielekeza kwenye kutafuta chanzo cha changamoto ya wanafunzi kutofanya vizuri kwenye mitihani yao ili kupata suluhisho la kudumu kwenye elimu na kwamba pamoja na kuendelea kuimarisha miundombinu watashirikisha wazazi na wahitimu wa vyuo vikuu kwenye kada ya elimu

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke Abdallah Mtinika ametaja changamoto ya lugha ya kingereza kama kikwazo cha ufaulu kwa wanafunzi huku Afisa elimu Mkoa wa Dar es salaam Bwana Gift Kyando akizungumzia changamoto ya usafiri kwa wanafunzi wanaosoma shule za mbali ambao wamekua wakiachwa vituoni na magari.