Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Mbeya
CHAMA cha Kulinda na Kutetea Haki za Walimu Tanzania (CHAKUWAHATA) wilayani Mbarali mkoani Mbeya kimetoa msaada wa taulo za kike 50 kwa wanafunzi wa shule za Sekondari Haruni na Mshikamano ili kuwasaidia wanafunzi wa kike wanaokabiliwa na changamoto ya kumudu gharama za kununua taulo hizo.
Msaada huo ulikabidhiwa wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika kata ya Igurusi.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Mwalimu wa Shule ya Msingi Manienga iliyopo kata ya Mawindi wilayani Mbarali, Janet Chacha, amesema walimu wameguswa kusaidia wanafunzi wa kike ili waweze kujisitiri na kujiamini wanapokuwa shuleni.

Amesema mpango huo utakuwa endelevu na kwa mwaka huu wameanza katika wilaya ya Mbarali, lengo likiwa kuwasaidia wanafunzi wa kike wanaoishi katika mazingira magumu ili waweze kuendelea na masomo yao bila vikwazo.
“Tunatoa wito kwa jamii inayowazunguka kuwasaidia watoto hawa waweze kujisitiri badala ya kukaa nyumbani wakati wa siku zao za hedhi kutokana na kukosa taulo za kike,” amesema Chacha.
Aidha, amesema Chama hicho kina jumla ya wanachama 748 katika wilaya ya Mbarali, ambapo wanawake ni 271 na wanaume 477.
Kwa upande wake, Mwalimu ,Victoria Sulumbu amesema waliona umuhimu wa kuwasaidia wanafunzi wa kike kutokana na changamoto wanazokumbana nazo, hasa wanapokuwa katika siku zao za hedhi.
Amesema mara nyingi wanafunzi wa kike hukosa vipindi vya masomo kutokana na kushindwa kujisitiri, hali inayochangia kurudi nyuma kitaaluma.
“Sisi kama chama tumeona kuna umuhimu wa kuwasaidia watoto hawa kulingana na mazingira wanayopitia. Tunatoa wito kwa jamii na wadau mbalimbali kujitolea kuwasaidia ili kumpa nguvu mtoto wa kike ambaye ni taifa la kesho aweze kusoma bila hofu,” amesema Sulumbu.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Haruni, Fatuma Kalua anayesoma kidato cha nne, aliwashukuru walimu hao kwa msaada huo na kusema taulo hizo zitakuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi wa kike.
Naye mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mshikamano, Gladness John, amesema taulo za kike huwasaidia wanafunzi wa kike kujisitiri na kujiamini wakiwa shuleni.
Amesema wakati wanapokosa taulo hizo hulazimika kukabiliana na mazingira magumu ambayo wakati mwingine huwafanya kushindwa kuhudhuria masomo.



More Stories
REA yapongezwa kuwawezesha wandelezaji wadogo wa miradi Umeme
Serikali kuendelea kupeleka huduma kwa Wananchi
Mvua yasababisha mafuriko Mwanza,watoto wanne waokolewa Mkuyuni