April 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CHADEMA yazidi kuwaka moto,Mchome amtaka Lissu akubali kukosolewa

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinazidi kuwaka moto wa ndani ya Chama huku Mwenyekiti wa Chadema, Wilaya ya Mwanga, Lembus Mchome amemtaka Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu kukubali kukosolewa na si kutukana wanachama.

Ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari, amesema ni muhimu Lissu akubali kukosolewa katika mambo anayoyafanya ili kuweza kujenga chama chao na kuwa imara.

“Hutaki kukosolewa umekuwa Mungu, kwanini tusikukosoe, tusikuseme na tusilete hoja mbadala ambazo wewe kama Mwenyekiti wa Chama Taifa unapaswa kukaa chini kuziangalia kama unaweza kuzipokea au kuzipuuza.

“Nimuombe Mwenyekiti wangu akubali kukosolewa ili tuijenge Chadema imara, taasisi yenye nguvu na kukuza umoja wetu tuliokuwa nao hapo awali, wala hana haja ya kututukana,” amesema Mchome

Akizungumzia kususia kwa uchaguzi Mchome amesema kuwa anaamini kuwa Chadema kisipoenda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kinaweza kufa na kupoteza imani.

Amesema matumaini waliyokuwa nayo watanzania kuwa Chadema ndicho chama cha upinzani kinachoweza kushindana na Chama cha Mapinduzi (CCM).


“Mimi ninaamini kwamba Chadema tusipoenda kwenye uchaguzi, tutakiua na kukimaliza chama hiki pia tutakichimbia kwenye kaburi hatutaweza kutoka tena, chama hiki tumekijenga kwa jasho kubwa sana na wengine tumekuwa wahanga wakubwa,mimi tangu mwaka 2007 nikiwa kijana mdogo nilijiunga nimetoa rasilimali zangu na kutumia mali zangu nyingi, hivyo hatuwezi kukubali kuona chama hiki kinakwenda kaburini.

“Leo mwenyekiti unasema wale ambao wanataka kushiriki katika uchaguzi wanatumika tuambie wanatumika na nani na kwa faida gani, na sisi tukisema wale ambao hawataki tushiriki uchaguzi mkuu ndio wanaotumika ili Rais Samia asipate upinzani mwaka huu tutakosea,” alihoji Mchome