November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CHADEMA, Reginald Munisi

CHADEMA yafungua dirisha uchukuaji fomu wagombea

Na Penina Malundo, TimesMajira Online, Dar es Salaam

CHAMA cha Demokrasia na Maendelea (CHADEMA) kimetangaza rasmi dirisha la uchukuaji wa fomu kwa wagombea wa udiwani, ubunge na urais ndani ya Chama kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba,mwaka huu.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CHADEMA, Reginald Munisi akizungumza na wanahabari (hawapo pichani)

Uamuzi huo ulifikiwa na Kamati Kuu ya CHADEMA iliyokutana mwishoni mwa wiki, ambapo kila mgombea atakayetangaza nia ya kuwania nafasi yoyote ndani ya Chama hicho atatakiwa kuhakikisha anafuata Sheria,Kanuni na Utaratibu wa Chama na kuhakikisha anajua kukisimamia Chama mahali popote.

Akitangaza kuanza kwa mchakato huo jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Chama hicho, Reginald Munisi amesema utahusisha kuangalia uwezo wa mgombea katika kusimamia Chama na kujitoa kikamilifu.

Amesema katika mchakato wa kumpata mgombea Urais wa Tanzania ndani ya Chama, mtia nia au wakala wake Julai 4,mwaka huu Chama hicho kitafungua mlango wa Mtia nia au wakala wake kuchukua fomu  za kugombea Urais wa Tanzania kupitia Chama hicho.

Amesema fomu hizo za urais zitatolewa Makao Makuu ya Ofisi ya Chama hicho na kila mgombea atatakiwa kudhaminiwa na wanachama wasiopungua 100 kwa kila Kanda.“Tunakanda 10 za CHADEMA Tanzania, nane zipo Bara na visiwani zipo kanda mbili, hivyo wagombea watapita na kuomba wadhamini katika kanda hizo na wadhamini hao hawapaswi kuwa ni wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Taifa,”amesema na kuongeza kuwa;

“Mgombea wa nafasi hiyo au wakala wake atatakiwa kuwasilisha fomu za kuomba uteuzi Julai 19 mwaka huu na kuambatanisha viambatanisho vyote vilivyotajwa katika fomu na stakabadhi ya malipo ya fomu kwa Katibu Mkuu wa Chama,”amesema Munisi.

Aidha amesema Jula 22, mwaka huu Katibu Mkuu wa Chama hicho atawasilisha taarifa kuhusu mchakato huo kwa kamati kuu ya chama ambapo Kamati hiyo itapendekeza jina au majina ya wagombea kwenda Baraza Kuu na Mkutano Mkuu kwa ajili ya mapendekezo ya uteuzi wa mwisho .

Akizungumzia upande wa nafasi ya ubunge, amesema wagombea wa ubunge watatakiwa kujaza fomu za kuomba uteuzi wa kugombea nafasi hiyo ndani ya Chama.

Amesema fomu zao zitatolewa Julai 4, mwaka huu hadi Julai 10 kwa Tanzania Bara na Visiwani ambapo zitapatikana katika mtandao wa chama na Ofisi za Majimbo ya Chama hicho.

“Kamati Kuu ya Chama itafanya uteuzi wa wagombea wa nafasi ya ubunge Julai 30 hadi 31 mwaka huu,ambapo wagombea wataitwa na kuhojiwa juu ya uanachama wao  na sera zao,”amesema na kuongeza

“Hatua ya pili majina yatakayoteuliwa yatapelekwa katika kura ya maoni kwa Mkutano Mkuu wa Majimbo kisha kurudishwa katika kamati tendaji ya Kanda na kufanya mapendekezo ya kugombea nani anafaa,”amesema

Akizungumzia nafasi za Udiwani

Munisi amesema utafiti wa kuwapata wagombea wa udiwani (Tanzania bara)utaendeshwa kwa kuzingatia sheria ya Chama huku kila mgombea akiitwa mbele ya kamati ya Utendaji kueleza taarifa zake.

Amesema fomu zao zitaanza kutolewa Julai 11, mwaka huu katika Ofisi za kata za Chama na kurudisha fomu Julai 17,mwaka huu nao watapigiwa kura ya maoni ambapo Kamati ya Utendaji ya Jimbo ambayo itakaa na kufanya uthibitisho wa wagombea udiwani .

“Katika upande wa fomu za viti maalum tarehe yao ya kuchukua fomu ni kama ile ya ubunge ni vema Watanzania kupata nafasi ya kumchagua mtu wanaomtaka katika kuwaletea maendeleo,”amesema