December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CHADEMA yaeleza kuhusu mgombea urais

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha CHADEMA kupitia kwa Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa chama hicho, Tumaini Makene, kimesema kuwa mpaka sasa hivi hakuna tangazo lililotoka ambalo, linawapa nafasi watangaza nia za kugombea Urais ndani ya chama hicho, kuwasilisha taarifa zao kwa Katibu Mkuu wa chama hicho.

Makene alitoa kauli hiyo jana wakati akihojiwa kwenye kipindi cha SupaBreakfast kinachorushwa na East Africa Radio.

Amesisitiza kwamba kuwa mwanachama yeyote wa chama hicho, hata kabla ya kutangaza nia ya kugombea ni lazima atakuwa ameisoma na kuilewa katiba ya CHADEMA.

“Lakini kabla ya kuwasilisha, katika sehemu ambayo unakuwepo kunakuwa na tangazo limetoka na watu wanapeleka makusudio yao ofisi ya Katibu Mkuu, halafu mchakato mwingine unafuata kwa mujibu wa taratibu za chama, na tangazo la watu kuwasilisha nia zao bado halijatoka,” amesema Makene.

Aidha Makene ameongeza kwamba wanaamini kuwa mtu yeyote ambaye ni mwana CHADEMA, anafahamu utaratibu kabla ya kutangaza nia ya nafasi hiyo kubwa kwamba atakuwa amesoma Katiba ya chama, kwahiyo wanaamini kwamba hakuna mtu atakayekiuka utaratibu huo”.

Kauli hiyo ya Makene imekuja ikiwa kuna taarifa kuwa mwanamke Dkt. Mayrose Majinge, ametangaza nia ya kugombea nafasi ya Urais kupitia CHADEMA.

Dkt. Majinge, akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza juzi amesema kuwa lengo la kuwania nafasi hiyo ni kutaka kuona Tanzania inakuwa taifa imara lenye watu wenye afya bora na wenye uhuru kamili.

Amesema tangu mwaka 2005 alianza harakati hizo akiwa miongoni mwa watia nia kuwania nafasi ya kugombea ubunge wa Jimbo la Ukonga, kabla halijagawanywa na kuwa majimbo mawili (Segerea na Ukonga), lakini kura hazikutosha jambo ambalo alidai limempa uzoefu mkubwa wa kisiasa.

“Nilipata uzoefu mwingine wakati nilipowania nafasi ya ubunge Bunge la Kwanza la Afrika Mashariki, ndiyo maana kwenye uchaguzi wa mwaka 2010 na 2015 sikuonekana katika ulingo tena, siyo kama niliacha kwa kutopenda ubunge, bali niliamua kujikita katika maandalizi ya kuwania nafasi ya juu ya uongozi wa nchi,” amesema Dkt. Majinge. .

Amesema uongozi ni dhamana ni lazima watu wakujue na kukuamini kwa kujitolea kusaidia katika nyanja mbalimbali ili waweze kukupa dhamana ya kuongoza nchi.

Dkt. Majinge amesema mwaka 2014/2019 alifanya kazi kubwa ya kuzuru nchi mbalimbali duniani kwa lengo la kujenga uhusiano wa kimataifa.