December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kusini ambaye pia alikuwa Mbunge wa Jimbo la Iringa, Mch.Peter Msigwa akipokea cheti cha heshima ikiwa ni ishara ya upendo kutoka wa wanachama wa chama cha CHADEMA

Chadema Iringa yawaaga Wabunge na Madiwani wao.

Na Zuhura Zukheir, TimesMajira Online, Iringa

WANACHAMA wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Iringa , wamewaaga Wabunge na Madiwani wa chama hicho waliohudumu katika kipindi cha miaka mitano bila kuhama chama hicho.

Wakizungumza katika hafla hiyo, wanachama hao wamesema madiwani na wabunge hao waliomaliza muda wao, wamewapa heshima kubwa katika utumishi wao, licha ya kupata maumivu makali kwa baadhi ya madiwani waliokuwa wamekisaliti chama hicho, wao wamewapa  heshima kubwa  ndani ya mkoa huo.

Mmoja wa wazee wa chama hicho, Mzee Haule amewataka viongozi chama hicho kuona haja ya kuwa na ofisi ya chama ya wilaya na mkoa badala ya mwanachama anapokuwa na shida   kushikana na viongozi barabarani.

“Ni aibu kwa chama chetu ambacho ni kikubwa kuwa hakina ofisi, miaka yote mkoani Iringa, hatuna Ofisi ya Wilaya wala Mkoa ni aibu kwetu sote, tunaomba sasa hivi kipaumbele iwe Ofisi ya Chadema ya Wilaya na Mkoa,” amesema Mzee Haule

Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kusini ambaye pia alikuwa Mbunge wa Jimbo la Iringa, Mch.Peter Msigwa amewataka wananchi kuchagua viongozi wenye malengo ya kulivusha taifa.

Mch.Msigwa amesema endapo jina lake halitapitishwa na chama chake katika kinyang’anyiro cha Urais hatasita kurudi kugombea Ubunge wa Jimbo la Iringa.

Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Iringa ambaye pia alikuwa Diwani  wa Kata ya Mivinjeni Mjini Iringa, Frank Nyalusi amesema siasa za msimu huu zilikuwa nzuri kwa upande wao.

Nyalusi amesema ni vema wasimamizi wa uchaguzi wakasimamia haki katika Uchaguzi Mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Ocktoba mwaka huu, ili mwenye kushinda ashinde kwa haki na mwenye kushindwa ashindwe kwa haki jambo ambalo halitaleta manung’uniko.

Meya wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe amesema katika uongozi wake alipitia wakati mgumu hasa lilipoanza wimbi la baadhi ya madiwani wa chama chake kuwa wasaliti na kujivua nyadhifa zao.

Kimbe ambaye pia ametangaza nia ya kugombea nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Iringa mjini amesema anawashukuru viongozi, wanachama pamoja na wapiga kura wa Kata yake waliokuwa wakimpa moyo wakati wote wa utendaji wake wa kazi.

Aidha Wabunge na Madiwani hao wamekabidhiwa vyeti vya heshima ikiwa ni ishara ya upendo.