November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM Zanzibar yapongeza hotuba ya Dkt. Rais Samia

Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraZanzibar

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt. Mohamed Said Dimwa, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa hotuba nzuri katika maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Polisi Tanzania, inayohimiza jeshi hilo kujitathmini na kujisahihisha ili liendelee kuaminiwa katika jamii.

Dkt. Dimwa,alisema hotuba hiyo imekuwa ni nasaha za kuongeza ari na utendaji wa jeshi hilo, lenye dhamana ya kulinda raia na mali zao na kwamba maisha ya wananchi yanategemea uwepo wa usalama na amani ya kudumu nchini.

Hayo aliyaeleza katika mahojiano maalum na vyombo vya habari wakati akichambua hotuba hiyo.

Alisema mafanikio ya uwepo wa amani na utulivu nchini ni juhudi za jeshi la polisi na kwamba linalotakiwa kuongeza juhudi zaidi kudhibiti vitendo vya uhalifu na kauli za uchochezi nchini.

Alisema Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kinampongeza kwa dhati hotuba ya Rais Dkt.Samia , ambayo imetoa muongozo kwa jeshi la polisi na majeshi mengine kujiimarisha zaidi kiteknolojia ili watekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Dkt. Dimwa, alisema kupitia hotuba hiyo Dkt.Samia alilitaka jeshi hilo liandae bajeti yenye mahitaji ya kujiimarisha na kujengewa uwezo kwa nyenzo na vitendea kazi vya kisasa vitakavyo waongezea mbinu za kisasa na atatekeleza mahitaji hayo kwa wakati.

Dkt. Dimwa, alifafanua kuwa Rais Samia, alilitaka la polisi kutofumbia kuwafumbia macho wale wote wenye nia ovu ya kuleta vurugu na uvunjifu wa amani.

Alisema hotuba hiyo iliyochukua zaidi ya dakika 57, ililitaka jeshi la polisi kuimarisha mbinu zake za kuzuia vifo vinavyotokana na ajali za barabarani,mauaji yanayohusisha wazi,viongozi wa dini,viongozi wa kisiasa na watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) kuhakikisha vitendo hivyo vinadhibitiwa.

Pamoja na hayo alisema katika uongozi wake hatoruhusu mataifa ya nje kuingilia uhuru wa nchi na Tanzania itaendelea kujiamulia mambo yake ya ndani kwa mujibu wa sheria zilizopo.

“Chama Cha Mapinduzi tunaunga mkono maelekezo yote yaliyotolewa na Rais Samia kwa Jeshi la Polisi kwani maendeleo yetu yataimarika kutokana na uwepo wa amani na utulivu, hatuwezi kupiga hatua yoyote kama nchi yetu ipo katika machafuko kwani wananchi watashindwa kufanya kazi na nchi itashindwa kujiendesha.”, alifafanua Dkt.Dimwa.

Sambamba na hayo alisema, hotuba hiyo ilienda mbali zaidi na kuvitaka vyama vya siasa kujitathimi na kuacha siasa za chuki na kiharakati badala yake wafanye siasa za kitaarabu zinazoleta ufanisi kwa nchi.

Dkt. Dimwa, alisema kila chama cha siasa kina dhima kubwa ya kuhakikisha sera zake zinakuwa ni rafiki kwa usalama wananchi na taifa kwa ujumla.

Alisema CCM hairidhishwi na baadhi ya kauli za viongozi wa vyama vya kisiasa kuanzisha kampeni za kulenga kuwachafua viongozi wakuu wa nchi kwa maslahi ya vyama vyao huku wakisahau maridhiano ya kisiasa yaliyoasisiwa mara baada ya kuingia kwa serikali ya awamu ya sita kwa ridhaa ya Rais Dkt.Samia.

Aliwambia wananchi kuendelea kuwa wamoja na kupuuza sera na hoja dhaifu za vyama vya upinzani zinazoibuliwa kila baada ya kukaribia uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.

“Wanasiasa tuepuke kuwa vyanzo vya kuratibu migogoro na mipango miovu dhini ya nchi yetu wenye, amani tuliyonayo nchi nyingi wanaitamani, uchaguzi unapita lakini Tanzania itabaki kuwepo kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.”alifafanua Dkt.Dimwa.

Kupitia uchambuzi huo Dkt.Dimwa, alitoa wito kwa vyama vya siasa nchini kuenzi na kuthamini uhuru wa kisiasa unaozingatia demokrasia uliopo nchini huku wakijisahihisha na kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa changamoto zao kupitia njia za mazungumzo na maridhiano kwa njia ya amani kabla ya kuingia katika uchaguzi mkuu wa dola.