December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM yataka maji yawafikie wananchi

Na Yusuph Mussa,Timesmajira Online,Korogwe

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Korogwe Mjini mkoani Tanga Thobias Nungu ametaka maji yanayozalishwa kutoka vyanzo mbalimbali vya maji kwenye Mji wa Korogwe, yawafikie wananchi badala ya kupotea njiani.

Amesema kwa sasa maji yanayozalishwa kwenye Mji wa Korogwe ni zaidi ya lita 5.5 kwa siku sawa na asilimia 88 ya mahitaji ya lita zaidi ya milioni 6.2 kutoka asilimia 32 iliyokuwepo kabla ya kutekelezwa kwa mradi wa maji Mashindei huku lita milioni 2.3 sawa na asilimia 39 ya maji hayo, yanapotelea kwenye mfumo.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Korogwe Mjini Thobias Nungu, akizungumza mbele ya Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji Korogwe huku Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Korogwe Nassoro Mohamed (kulia), na Katibu wa CCM Wilaya ya Korogwe Mjini Evarest Mluge (kushoto)

Nungu ameyasema hayo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji Korogwe,ambapo ameeleza kuwa ndiyo maana bado kuna malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi kuwa hawapati maji hiyo ni kutokana na maji hayo kupotelea kwenye mfumo.

Ameeleza kuwa jitihada zinatakiwa kufanyika ili kuhakikisha maji yanayozalishwa hayapotei kwenye mfumo ni kweli kwa sasa uzalishaji wa maji kwenye Mji wa Korogwe kwa siku ni asilimia 88 ya mahitaji lakini asilimia 39 ya maji hayo, yanapotelea kwenye mfumo, hivyo kufanya wananchi kupata lita takribani milioni 3 sawa na asilimia 54.

“Tunataka kuona tatizo hilo la kupotea maji linapatiwa ufumbuzi wananchi wanapata maji kwa hiyo asilimia 88 ya ukweli, kwani kilio chao cha kutaka maji kwenye Mji wa Korogwe kipo maeneo mengi,” amesema Nungu.

Mhandisi Bahati Ngowi akitoa taarifa ya upatikanaji maji Mji wa Korogwe kwenye Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji Korogwe

Akijibu hoja hizo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji waHandeni Trunk Main(HTM) Mhandisi Yohana Mgaza,ambao walipewa jukumu na serikali la kusimamia miradi ya maji Korogwe Mjini Mhandisi Bahati Ngowi amesema sababu ya asilimia 39 ya maji yanayozalishwa kupotea, ni uchakavu wa miundombinu ya maji kwenye Mji wa Korogwe ambayo tangu ijengwe ni zaidi ya miaka 50 iliyopita.

“Mambo matatu yanachangia kupotea kwa maji kwanza ni uchakavu wa miundombinu ya maji hasa mabomba,pili ni baadhi ya wateja wasio waaminifu kufungua mita huku wengine kujiunganishia maji kijanja bila kutumia utaratibu na tatu, baadhi ya mita ni mbovu tunafanya jitihada kuondoa changamoto ya upotevu wa maji,” amesema Mhandisi Ngowi.

Mhandisi Ngowi amesema ili kumaliza changamoto za maji kwenye Mji wa Korogwe mipango ya muda mfupi ni kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji Mashindei kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa maji.

Pia kubadili dira (mita) za maji ambazo ufanisi wake umepungua, kuboresha miundombinu ya kusambaza maji kwa kulaza bomba lenye urefu wa kilomita 24.9 katika Mji wa Korogwe.

Huku mipango ya muda mrefu ni ujenzi wa mradi wa maji kwa kutumia chanzo cha Mto Ndemaha ambapo litajengwa dakio, na kulaza bomba urefu wa kilomita 21,
kutekeleza ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji lenye uwezo wa kujaza lita milioni 2, eneo la Kwamkole,miundombinu ya kusafisha, kuchuja na kutibu maji eneo la Kwamkole kwa ajili ya kuhakikisha maji yanawafikia wananchi yakiwa safi na salama tofauti na ilivyo hivi sasa.

Madiwani wa Halmashauri ya Mji Korogwe wakiwa kwenye kikao cha Baraza

Pamoja na kujenga nyumba ya maabara katika eneo la Kwamkole,utekelezaji wa mradi wa Miji 28, ambapo Mji wa Korogwe ni moja ya miji itakayonufaika na mradi huo.

“Mkandarasi tayari ameanza utekelezaji wa mradi kwa kufikisha mabomba kwenye baadhi ya maeneo na zoezi la kulaza mabomba na ujenzi wa matenki limeanza,” amesema Mhandisi Ngowi.

Ngowi amesema mamlaka inahudumia wakazi wa Korogwe kutoka kwenye vyanzo vya maji vya Mto Mdogo wa Mbeza, Mto Mashindei, Mto Pangani (eneo la Mtonga na Old Korogwe) na visima virefu 6 vilivyopo maeneo ya Majengo, Kwasemangube, Mbeza mawe, Manzese, Kwameta, Kwakombo na chanzo cha HTM kinachohudumia kata ya Mgombezi.

Miundombinu ya utoaji wa huduma ya maji katika Mji wa Korogwe inajumuisha vyanzo 10, matanki 15 yenye jumla ya mita za ujazo 3,100 na mtandao wa mabomba wenye urefu wa kilomita 156 huku Mamlaka ya Maji Korogwe ina maunganisho ya wateja wapatao 5,497, wote wamefungiwa dira za maji na upotevu wa maji ni wastani wa asilimia 39.

” Oktoba, 2023 mamlaka imekusanya zaidi ya milioni 38.8 kutoka katika maduhuli ya maji, maunganisho mapya na kurudisha huduma pia haijapokea fedha kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi.

Baadhi ya watumishi wakiwemo Watendaji wa Kata waliohudhuria kikao cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji wa Korogwe

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake, Mkurugenzi Mtendaji wa HTM, Mhandisi Yohana Mgaza, amesema dira (mita) za maji 2,000 zimeshanunuliwa kwa ajili ya kuwafungia wateja kwenye Mji wa Korogwe.

Hivyo muda si mrefu changamoto za upotevu wa maji itabaki historia, sababu tayari watakuwa wameshaweka miundombinu mipya ikiwemo mabomba.