November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM yataka hatua thabiti ripoti ya CAG

Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam

KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa,imepokea na kujadili kwa kina masuala mbalimbali ya kitaifa, ikiwemo taarifa zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kwa mwaka wa fedha 2021/22, zilizowasilishwa kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, hivi karibuni na kuitaka Serikali kuchukua hatua thabiti kwa wahusika wote waliobainika kuhusika katika ukiukaji wa sheria na kusababisha ubadhirifu wa mali na rasilimali za nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam,Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa – Itikadi na Uenezi,Edward Mjema amesema kupitia taarifa hizo zimeonyesha Serikali imeboresha na kuendelea kuimarisha kasi ya utoaji wa huduma kwa wananchi, ikiwemo udhibiti na umakini katika matumizi ya fedha za umma, ambapo katika taasisi zilizokaguliwa, asilimia 96 zimepata hati safi.

Amesema Ofisi hizo zimefanya kazi kubwa kwa weledi na kuendelea kutimiza wajibu wao kwa taifa, kwa kuonesha maeneo ambayo Serikali imeyaboresha na kubainisha madhaifu yanayohitaji kufanyiwa kazi, kwa lengo la kulinda mali, rasilimali kwa maslahi ya taifa.

“Kamati imesikitishwa na kuwepo baadhi ya maeneo mengine ambayo bado yanatakiwa kufanyiwa kazi ili kuondoa mapungufu na udhaifu uliobainishwa, ikiwa ni pamoja na mifumo ya malipo na ukusanyaji wa mapato kutokusomana, kuwepo kwa baadhi ya watumishi wa umma wasiokuwa waadilifu, hali inayosababisha serikali kukosa mapato na kupata hasara, uwepo wa mashirika ya umma yanayojiendesha kwa hasara na vitendo vya ubadhirifu wa mali na rasilimali za umma, kama vile kuongeza bei za manunuzi ya Serikali”ameswma na kuongeza

“Kutokana na haya yaliyobainika Serikali ihakikishe inawafatilia watu wote wanaotumia dhamana za uongozi vibaya na kushindwa kuweka maslahi ya nchi na uzalendo mbele katika nafasi walizoaminiwa kutumikia watu, badala yake wanaweka maslahi binafsi,”amesema.

Aidha Mjema amesema Kamati hiyo imeipongeza Serikali kwa kuratibu na kufanikisha vema ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani,Harris Kamala aliyetembelea nchi ya Tanzania kwa siku tatu.

Amesema ziara hiyo imeongeza uimara wa ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani na kufungua milango zaidi ya mahusiano yenye faida kwa maendeleo na ustawi kwa pande zote mbili, hususan katika maeneo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, kukabiliana na magonjwa, uchumi, uwekezaji na ajira.