March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM yasisitiza wagombea kujadiliwa kwa kuzingatia uwezo

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online

KATIBU wa NEC – Oganaizesheni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Issa Ussi Gavu,amewataka Wajumbe wa Halmashauri Kuu za CCM Wilaya, mkoani Iringa, kukijenga chama kwa kusimamia misingi imara, hususani kwa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Ambapo amesisitiza kuwajadili wagombea wa nafasi za Ubunge na Udiwani kwa kuzingatia uwezo, sifa nzuri, uadilifu, uzalendo na si kuweka mbele ukabila, undugu na urafiki.

Gavu amesema, hayo wakati akifungua mafunzo maalumu ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu za CCM za Wilaya katika Mkoa wa Iringa, yaliyokuwa na lengo la kuendelea kukijenga chama katika misingi imara na thabiti.

Akiziungumza na Wajumbe hao, Gavu amewataka viongozi ngazi ya Mkoa, WIlaya na Kata,wakati utakapofika wa kujadili majina ya wagombea, wajadili kwa kuzingatia uwezo, sifa nzuri, uzalendo na uadilifu na si kwa kuweka mbele ukabila, urafiki wala undugu kwakuwa CCM akihusudu hayo.

Gavu amesema, iwapo mgombea ana sifa za kugombea na anakubalika na jamii, apewe kipaumbele bila kujali ni adui kwa baadhi ya wajumbe, huku akisema kuwa, kikao kinatakiwa kimpendekeze kwakuwa huyo atafaa kuwa mgombea kwa maslahi ya Chama Cha Mapinduzi na Taifa kwa ujumla, na iwapo mgombea hana sifa na hakubaliki kwenye jamii hata kama ni rafiki wa wajumbe hatakiwi kupendekezwa na kikao husika

“CCM inataka vikao vyake kwa ngazi zote vitoe mustakabali mzima wa maendeleo kwa watanzania kwa ujumla kwa kuwapata wagombea walio tayari wakati wowote kujikosoa, kukosolewa na kukosoana.Natoa onyo kali kwa kikao chochote kile kuweka au kutangaza msimamo kwa nafasi yoyote inayogombewa iwe Ubunge ama Udiwani na badala yake misingi ya Haki, Usawa na Uwazi izingatiwe”. Amesema Gavu.

Aidha, Gavu amesema vikao vitatakiwa kuzingatia aliyeongoza kwa kura za maoni isipokuwa kama iwapo itabainika wazi kuwa kura hizo alizipata kwa njia ya rushwa basi katika mchujo kikao hakitamteua kugombea nafasi aliyoiomba na lazima aelezwe wazi tuhuma zake.

Akihitimisha katika hotuba yake, Gavu amesema vikao vyote vya uchujaji na uteuzi vizingatie mujibu wa Katiba na Kanuni za CCM, ambapo amesema CCM inaendelea kuwasihi wajumbe kuzingatia miiko na misingi ya CCM ili kutimiza lengo la Ibara ya 5 la kushinda katika chaguzi zote.