Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
KATIBU Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza,Prudence Sempa amesema ziara ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM Itikadi na Uenezi,Paul Makonda,iko pale pale na atawasili mkoani Mwanza Jumamosi Novemba 11,2023.
Sempa amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza Novemba 9,2023 ambapo ameeleza kuwa Makonda atawasili mkoani humu saa 4:00 akitokea mkoani Geita kwa ajili ya ziara yake ya siku tatu atapokelewa na viongozi wa Chama na Serikali katika Kijiji cha Kilabela,wilayani Sengerema.
Ambapo atavishwa skafu na kisha ataelekea katika soko la zamani la Sengerema kusalimia wananchi na wanaCCM ataelekea Busisi ambako atapata taarifa ya serikali kuhusu maendeleo ya mradi wa daraja la J.P. Magufuli hatua ulipofikia.
Hivyo kwa ilivyo desturi wananchi,wanaCCM na wakereketwa wajitokeze kumlaki kiongozi huyo ambapo atasikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi pamoja kukiimarisha chama.
“Baada ya kupokea taarifa ya serikali,Makonda na msafara wake atavuka kupitia daraja hilo la J.P Magufuli kuelekea Misungwi ambapo atapokelewa na viongozi,waendesha bodaboda na makundi mengine hadi Usagara ambako atatawazwa kuwa ‘Nsumba Ntale’ yaani kijana mkubwa kupewa mamlaka ya mila za Wasukuma,niwahakikishie ziara yake iko pale pale na hivyo wasisikilize taarifa za upoyoshaji.
Pia amesema Makonda (Nsumba Ntale) atapewa heshima hiyo na wananchi wa Misungwi wakiwemo Machifu kwa kutambua utendaji kazi wake imsaidie katika shughuli zake za kuwatumikia wananchi kitaifa.
Ameeleza kuwa Makonda Novemba 12 atakutana na Kamati ya Siasa ya Mkoa,kisha atazungumza na Wazee wa Jiji la Mwanza pamoja na Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini katika Ukumbi wa Chuo cha Benki Kuu (BOT).
Kwa mujibu wa Sempa mkutano wa hadhara utafanyika mbele ya jengo la CCM Mkoa wa Mwanza majira ya saa 8:00 mchana,umelenga mambo mawili,moja kusikiliza kero za wananchi na pili kutoa maelekezo ya utekelezi wa Ilani ya Uchaguzi kwa Serikali ambapo amealikwa Mkuu wa Mkoa,Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi wa Halmashauri na wataalamu.
“CCM inafanya kazi ya kutatua kero za wananchi ndiyo maana ya kuitisha mkutano wa hadhara ambao Makonda atautumia kutatua kero zao,kutoa maelekezo kwa serikali kuhusu utekelezaji wa ilani,hivyo wenye kero wafike wakiwa na vielelezo vyao,watapata fursa ya kusikilizwa na baadhi zitatatuliwa papo hapo na zingine zitatolewa maelekezo,”amesema.
Hata hivyo ameeleza kuwa hadi sasa maandalizi ya mapokezi ya Katibu huyo wa Itikadi, yamefikia asilimia 95 na kutakuwa na wasanii kama Oscar Nyerere,Muumini Mwijuma,vikundi mbalimbali vya ngoma na burudani,hivyo wanaCCM, wananchi,wajasiriamali,bodaboda na makundi mengine wakaribishwa.
Makonda ambaye Mwanza ni nyumbani atakuwa na hisia mchanganyiko ambapo atapata fursa ya kukutana na wananchi,atahitimisha ziara yake Novemba 13,asubuhi kwa kuzungumza na wananchi wa Kisesa wilayani Magu,kisha atasindikizwa kuelekea mkoani Simiyu kuendelea na ziara mkoani humo na atapokelewa viongozi wa Chama na Serikali katika eneo la Lamadi,wilayani Busega.
More Stories
Kyobya: Watakaohusika kudhoofisha jitihada za Serikali,Pori la Akiba Kilombero kushughulikiwa
Wenje:Tuwanadi wagombea bila kuchafuana
Mtoto darasa la tatu adaiwa kujinyonga kwa kukosa nguo ya sikukuu