June 3, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM yampongeza Rais Samia kutunukiwa tuzo na Bunge

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutunukiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tuzo maalumu ya heshima.

Tuzo hiyo iliyokabidhiwa na Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson Mei 31, 2025, imeelezwa kuwa ni kielelezo cha kuthibitisha mchango wenye matokeo chanya kwa kazi ambazo zimeendelea kufanywa na Rais kwa taifa.

Katika taarifa iliyotolewa na chama hicho chini ya Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, imeelezwa kuwa, tuzo hiyo inaonesha kuthaminiwa kwa uongozi wake unaojengwa kwa misingi ya amani, maridhiano ya kisiasa, mshikamano kitaifa na maendeleo endelevu kwa jamii na uchumi kwa taifa.

Aidha imeelezwa kuwa, chama hicho kinajivunia juu ya uongozi wa Rais Dkt. Samia kwa kuendelea kudhihirisha uimara, umakini na weledi wa CCM katika kutoa uongozi thabiti kwa taifa.

Pia katika taarifa hiyo imeelezwa kuwa, CCM inaunga mkono juhudi zinazofanywa na Dkt. Samia na kuwa kina imani nae katika kuendelea kuliongoza taifa.