December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM yakemea Wakandarasi kuongezewa muda kinyume na mkataba

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),Wilaya ya Nyamagana imewataka wataalamu na wahandisi kuwasimamia kwa weledi wakandarasi waotekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati wilayani humo ili kazi zifanyike usiku na mchana kuepuka kuongezwa muda.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Peter Bega wakati wa ziara ya kamati hiyo ilipotembelea kukagua miradi ya kimkakati ukiwemo wa uboreshaji wa Bandari ya Mwanza Kaskazini.

Amesema miradi ya kimkakati mikataba kuongezwa muda kinyume cha makubaliano sababu zinakuwa nyingi hivyo CCM hairidhishwi na hatua hiyo kwani wapo wabadhirifu wanaofanya hivyo ili kujinufaisha.

Ameipongeza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Kanda ya Ziwa kwa usimamizi mzuri uliomwezesha mkandarasi kufikisha asilimia 37 ya mradi wa uboreshaji wa bandari.

“Kwa fedha hizo sh. bilioni 18 si ndogo,ili kuiwezesha meli ya MV. Mwanza ianze kutoa huduma kwa wananchi kazi ifanyike usiku na mchana gati likamilike kwa wakati,tukifanya kwa bidii tutaiheshimisha serikali na CCM,tuna imani kubwa mradi huu utakamilika kwa wakati wananchi wapate huduma na watu wafanye biashara kwa kupeleka bidhaa nje na kuleta ndani kutoka nje ya nchi jirani za Kenya na Uganda,”amesema Bega.

Mwenyekiti huyo wa CCM amemtaka mkandarasi kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation(CR15G) kufanya kazi usiku ili meli ya MV. Mwanza ambayo tayari imekamilika iweze kutia nanga katika Bandari ya Mwanza Kaskazini,kinacholewesha ni uboreshaji wa upanuzi wa bandari hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi amesema mradi huo ni mzuri unatekelezwa kwa mujibu wa mkataba ambapo Rais Dkt.Samia ameendelea kutoa fedha ili ukamilike na kuwahudumia wananchi na kuleta manufaa ya kiuchumi na kijamii.

Amesema utekelezaji wa miradi hiyo ya kimkakati ni agenda ya serikali kuhakikisha inakamilika wananchi wapate huduma ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa vitendo.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo wa Uboreshaji na Upanuzi wa Bandari ya Mwanza Kaskazini,Meneja wa TPA Kanda ya Ziwa, Erasto Lugenge, amesema TPA katika mwaka wa fedha 2023/24 ilitenga fedha zaidi ya bilioni 18.6 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo ambao umefikia asilimia 37 na utakamilika Novemba 2024.

Amesema asilimia hizo zilizofikiwa zinahusisha ujenzi wa maegesho ya meli,miundombinu ya barabara na sakafu ngumu,jengo la abiria na la pampu ya mafuta,miundombinu ya kuhifadhia mafuta na mifereji ya maji.

Kazi zingine ni ujenzi wa jengo la ukaguzi wa abiria na mizigo,uzio wa bandari,kuweka miundombinu ya umeme,kuhamisha miundombinu ya reli na madaraja katika Bandari ya Mwanza Kusini na ujenzi wa kingo za Mto Mirongo.

“Changamoto zinazoathiri utendaji katika Bandari za Ziwa Victoria ni kina cha maji kuongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi, ufinyu wa eneo la shughuli za mradi kutokana na shughuli zisizo za bandari zinazoendeshwa jirani na bandari maeneo ambayo kisheria yanapasa kuwa chini ya usimamizi wa TPA,”amesema Lugenge.

Amesema katika kuchagiza maendeleo kwa wananchi TPA imejipanga kutekeleza mipango mbalimbali ya serikali kulingana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025-2050 na Ilani ya CCM 2020-2025 ili kutumia fursa za jiografia ya Mkoa wa Mwanza.

Lugenge amesema moja ni kuhakikisha mradi wa uboreshaji na upanuzi wa Bandari ya Mwanza Kaskazini unakamilika kwa wakati,kuendelea kutoa huduma kwa watumiaji wa bandari hiyo kipindi chote cha uboreshaji na baadae.

Pia kuendelea kushirikina na uongozi wa chama na serikali ngazi zote katika kufutailia utekelezaji wa mradi, kumsimamia mkandarasi ili kuhakikisha ajira zinazotolewa zinawanufaisha wakazi wa maeneo jirani ulipo mradi.