Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online,Songwe.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Songwe kimewataka makada wake wanaojipitisha kwa wapiga kura kabla ya wakati wa kampeni,kuacha mara moja, kikisisitiza kuwa chama hicho kina “macho na masikio makubwa mno” yanayofuatilia kila hatua.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo Mkoa wa Songwe, Mwalimu Yusuph Rajab,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maamuzi ya vikao vya maadili vilivyoketi kujadili migogoro ya ndani ya chama hicho, ikiwemo mgogoro kati ya Mbunge wa Momba, Kondesta Sichalwe, na Umoja wa Vijana wa Chama hicho (UVCCM) Wilaya ya Momba.
“Tupo kwenye mwaka wa uchaguzi,chama chetu kina utaratibu wa kuomba nafasi, kuwapitia waombaji na uteuzi, lakini sasa tunaona kuna watu wanajipitisha kwenye majimbo na kata.CCM ina macho na masikio makubwa mno, tunawaona, tunawasikia, na tunawafuatilia,”amesema Rajab.
Rajab amesema wanachama hao,wanapaswa kuelewa kuwa chama hakitavumilia uvunjaji wa taratibu, na kwamba hatua zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kufanya kampeni za mapema.
“Sio kwamba hatujui, tunafuatilia kila hatua na watambue kuwa majina yanayorudi ni matatu tu safari hii tuko makini kuliko wakati mwingine wowote,”.
Pia amesisitiza kuwa CCM itaendelea kushikiria misingi yake ya nidhamu, utii na maadili,chama hakitakuwa na masihara kwa wale wanaokiuka taratibu zake.
“Tunasema wazi, tusije kulaumiana. Utaratibu wa ndani ya chama chetu uko wazi. Tufuate sheria, mila na utamaduni wa CCM,” alihitimisha.
More Stories
Mpango ujenzi wa nyumba ya Katibu Jumuiya ya wazazi kuanzishwa
Waandikishaji wapiga kura watakiwa kuzingatia weledi
Serikali yasisitiza utamaduni wa kujikinga mahali pa kazi