May 17, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM kufanya mkutano mkuu maalumu Mei 29-30,2025

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online,Dar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza rasmi kuwepo kwa mkutano mkuu maalumu wa CCM Taifa, utakaofanyika Mei 29 hadi 30,mwaka huu Jijini Dodoma.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar-es-Salaam Mei 17, 2025, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo (CCM) Taifa, CPA. Amos Makalla, amezitaja ajenda tatu zitakazowasilishwa katika mkutano huo,ajenda kuu ikiwa ni kupokea na kuzindua rasmi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025/2030,itakayotumika katika kipindi cha kampeni za chama.

Ajenda nyingine ni kupokea Ilani ya CCM ya kipindi cha miaka mitano 2020/ 2025 Tanzania Bara na Zanzibar na nyingine ikiwa ni kufanyika kwa marekebisho madogo ya katiba ya chama hicho.

Pia amesema kuwa, CCM inaamini katika kushinda kwenye uchaguzi mkuu kutokana na kuwa na ilani inayokidhi mahitaji ya wananchi katika vipindi vyote.

Aidha ameipongeza Serikali kwa kutoa fedha nyingi za maendeleo, katika sekta ya afya, elimu,miundombinu ya barabara,maendeleo ya jamii na nyingine.