Na Penina Malundo, Timesmajira
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema chama chao kitahakikisha kinayaenzi yale yote yaliyosimamiwa na Rais Mstaafu wa ya awamu ya tatu Hayati Dk. Benjamin Mkapa kwa kujitolea kwake katika kutumikia nchi.
Dk.Nchimbi aliyasema hayo leo wakati alipotembelea na kuzuru kaburi la hayati Rais Mkapa katika Kijiji cha Lupaso, Masasi Mkoani Mtwara, katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tano kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara.
Balozi Dk. Nchimbi amesema hayati Mkapa alikuwa mfuatiliajia wa shughuli za maendeleo na kufanya mabadiliko makubwa kwa Watanzania. Amesema CCM chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan watahakikisha wanaendelea kuyaenzi yale yote yaliyoachwa na Hayati Mkapa.
Dkt. Nchimbi amesema kuwa urithi wa Mkapa ni wa kudumu na alibainisha nafasi yake muhimu katika mageuzi yaliyoboresha taasisi za serikali.
“Mkapa alihusika sana katika kuanzisha mageuzi yaliyoleta mabadiliko katika utawala,” amesema.
Amesema kwamba serikali inayoongozwa na CCM chini ya Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuthamini maisha na urithi wa Mkapa na kuhakikisha kuwa maono yake yanatimizwa.
“Hayati Mkapa alikuwa mzalendo kwa nchi yake, alifanya mabadiliko makubwa kwa nchi na CCM chini ya Rais na Mwenyekiti Dk. Samia Suluhu Hassan tutaendelea kuyaenzi yale yaliyoachwa na Hayati Mkapa, ” amesema.
***Akielezea uhusiano wake na Hayati Rais Mkapa
ADkt. Nchimbi ameelezea uhusiano wake na Mkapa, amesema hayati Mkapa alikua kama mwalimu wake wa kisiasa aliyeunga mkono elimu yake kifedha.
Amesema yeye akiwa miongoni mwa wasaidizi wake kupitia UVCCM, alifanya naye kazi kwa miaka saba akiwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM, alipenda kufuatilia hadi masuala ya elimu.
“Naomba nikiri kuwa mimi ni mwanafunzi wa hayati Mkapa na nimekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Taifa katika kipindi chake kwani ndio alinilipia ada ya kusoma Chuo Kikuu na alikuwa mfuatiliaji sana na alitulea na sio sisi lakini kwa Watanzania wote aliwalea.
Katika ziara hiyo Katibu Mkuu wa CCM ameambatana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa-NEC, Oganaizesheni, Issa Usi Haji Gavu, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA- Amos Makalla na Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa-SUKI- Rabia Hamid
More Stories
Waziri Mavunde:Benki Kuu yanunua tani 2.6 za Dhahabu nchini
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25