NA Heri Shaaban, TimesMajira Online
Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Ilala kimeadhimisha miaka 45 ya kuzaliwa kwake kwa kufanya ziara ya kukagua utekelezaji wa ilani kwenye sekta ya elimu.
Ukaguzi huo ulifanywa na wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM Kata ya Ilala ambapo walikagua ujenzi wa vyumba 17 vya madarasa katika Shule za Sekondari Mivinjeni na Msimbazi yaliyotokana na fedha za Uviko – 19.
Akizungumza wakati wa kukagua vyumba hivyo Mwenyekiti wa CCM Kata ya Ilala, Habibu Nasser, amezipongeza shule hizo kwa usimamizi mzuri wa fedha hizo.
“Tumekagua madarasa yaliyojengwa kwa fedha za Uviko – 19 kweli tumeona, tunawapongeza kwa usimamizi mzuri wa fedha na kujenga kwa ubora,” amesema Nasser.
Aidha amewataka wananchi kama kuna kero hazijafanyiwa kazi wasisite kuziwasilisha kwa viongozi wa chama ili ziweze kutatuliwa.
Naye Diwani wa Kata ya Ilala, Saad Khimj ambaye pia ni Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, amesema madarasa hayo yatamaliza changamoto ya wanafunzi kurundikana darasani na kuboresha ufundishaji.
Amesema pia wametenga Sh milioni 45 kwa ajili ya ujenzi wa matundu 10 ya vyoo katika Shule ya Sekondari Mivinjeni na kwamba kati ya fedha hizo Sh milioni 25 zitatoka halmashauri na Sh milioni 20 zitatolewa kupitia Mfuko wa Jimbo la Ilala.
“Kuna changamoto ya upungufu wa viti na meza za walimu pamoja na madawati, tunawahakikishia baada ya muda watoto wote watakaa katika mazingira mazuri na changamoto zote zitakwisha,” amesema Khimj.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Mivinjeni, Imani Kundema, amesema walipokea Sh milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 10 ikiwemo chumba cha maabara na kwamba vyote vimekamilika na tayari vimeanza kutumika.
Kwa mujibu wa mkuu huyo ujenzi wa vyumba hivyo umeongeza idadi ya wanaunzi wa kidato cha kwanza ambapo mpaka sasa tayari wamepokea wanafunzi 235 kati ya 328 waliochaguliwa kujiunga na shule hiyo.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Msimbazi, Pantaleo Maghali, amesema walipokea Sh milioni 140 za ujenzi wa vyumba saba na kwamba tayari vimekamilika na kuanza kutumika.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote