November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM inadhamira ya kumtua Mwanamke ndoo kichwani

Na Mwandishi wetu, timesmajira

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, Mary Chatanda, amesema Serikali ya CCM imeandaa bajeti kubwa ya kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji nchini ikiwemo Wilaya ya Kondoa  mkoani Dodoma lengo likiwa ni kumaliza kero ya maji.

Akizungumza leo Novemba 22, 2023 katika ziara yake ya siku moja ndani ya wilaya ya Kondoa Mwenyekiti Chatanda amewaomba wanawake kuendelea kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa na dhamira ya kumtua mwanamke ndoo kichwani kwa kuongeza miundombinu ya upatikanaji wa maji safi na salama majumbani.

Mwenyekiti Chatanda ameyasema hayo alipotembelea mradi wa usambaji Maji Kondoa Mjini,mradi uliogharimu zaidi ya shilingi Bilioni 4 zinazotumika katika Ujenzi wa Tanki ya Maji lenye ujazo wa lita 1,200,000

“Serikali ya awamu sita ina lengo kubwa la kuhakikisha inamtua ndoo mama kichwani katika kuwapatia huduma ya maji safi na salama kila kijiji, kitongoji na kata.

Aidha Chatanda ametembelea Chemchem ambayo ndio chanzo cha Maji Kondoa Mjini ambayo iliyogunduliwa zaidi ya miaka ya 70 iliyopita  amevutiwa na historia ya chanzo cha maji na kushauri waandaliwe watu wengine kwa ajili ya  kuijua historia ya eneo hilo ili iwe endelevu na kuwahudumia wananchi.

“Naomba nishauri Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mjini Kondoa kuhakikisha kabla ya kuendeleza chanzo hicho wawashirikisha wazee wa Kimila katika eneo hilo  ili kutopoteza asili ya eneo hilo,”amesema