December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCBRT yaadhimisha siku ya mguu kifundo Duniani

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Tafiti zinaonesha Dunia nzima takribani watoto laki nane katika vizazi hai wanazaliwa wakiwa na tatizo la mguu kifundo huku ikiripotiwa kuwa kwa Tanzania inakadiriwa watoto 3000 kila mwaka wanazaliwa wakiwa na tatizo hilo.

Hayo ameyasema Mganga Mkuu wa CCBRT, Cyprian Ntomoka wakati wakiadhimisha siku ya Mguu kifundo Duniani ambayo huadhimishwa kila tarehe 3 Mwezi Juni ya kila mwaka na kuongeza kuwa wengi wa watoto hao wanapatikana katika nchi ambazo zenye uchumi mdogo na kwa Tanzania wengi wao hupatikana hasa vijijini.

Dkt. Ntomoka amesema CCBRT inaadhimisha siku hiyo ili kuikumbusha jamii na kwa watu wote kwa ujumla kuhusiana na tatizo hilo la mguu kifundo ambapo wasipofanya hivyo kunauwezekano mkubwa baada ya miaka kadhaa ijayo kuwepo kwa watoto ambao wanaweza wakawa na miguu kifundo

Dkt. Ntomoka amesema Kwa mwaka, kwa makadirio wanafanya matibabu kati ya watoto 350-400 wapya ambao wanajiunga na matibabu ya CCBRT;

“Matibabu haya yanaweza kuchukua muda wa hadi miaka mitano, tukigundua tatizo hili kwa mtoto kuanzia alivyo mchanga akipatiwa matibabu anatakiwa aendelee kuja kufuatilia matibabu kwa zaidi ya miaka minne au mitano”

Pia Dkt. huyo amesema Kuanzia mwaka 2021 Julai mpaka Mei 2022 wamepata wagonjwa 306 wapya katika hospitali hiyo.

Mbali na hayo, Dkt. huyo amesema kama mtoto asipotibiwa mguu kifundo, akishakuwa mtu mzima akitembea mguu unakua unaingia ndani na anakosa ujasiri wa kuchangamana na watu wengine na kufanya shughuli nyingine za kitaifa.

Kuhusu changamoto kubwa ambazo wanakutana nazo, Dkt. Ntomoka amesema ni watoto kuchelewa kuja hospitali kwaajili ya matibabu.

Dkt. Ntomoka amewasihi watu wote wanaohusika na uzazi inapotokea amezalisha mtoto au mtoto amezaliwa na mguu kifundo mapema afanye mkakati wa kuwaona wataalamu ikiwezekana kuja CCBRT kuweza kufanya matibabu mapema

Kwa upande wake Dkt. wa idara ya mifupa, Frank, amezitaja Sababu ambazo zinapelekea mtoto kupata mguu kifundo ikiwemo kurithi, jinsi mtoto anavyokaa wakati wa ujauzito tumboni, wakati wa ujauzito mama kutumia kilevi au dawa ambazo hazijathibitishwa na wataalamu n.k

Aidha Dkt. Frank ametoa wito kwa wajawazito wawe wanapata lishe bora, wasitumie vilevi wala dawa ambazo hazijathibitishwa na wataalam lakini pia watakapojifungua wazazi wote wawachunguze watoto wao hasa kwenye miguu kama imekaa vizuri au inakifundo

Kwa upande mwingine ametoa wito kwa wakunga, wauguzi na madaktari ambao wanawazalisha wakina mama wahusike pia katika kuchunguza miguu ya watoto hao na endapo watabaini wanamguu kifundo wawalete CCBRT ili waanzishe matibabu mapema.

Naye mmoja wa wazazi mwenye mtoto mwenye mguu kifundo Hilda, amesema tangu alivyompeleka mtoto CCBRT kwaajili ya matibabu ya mguu kifundo mtoto amekuwa akiendelea vizuri kutokana na huduma bora ambazo anapatiwa hospitalini hapo hivyo amewasihi wazazi wengine kutoona aibu na kuwafungia watoto nyumbani bali wawachukue na wawapeleke CCBRT ili wapate matibabu sahihi na yaliyo salama

Mguu kifundo unatibika endapo mtoto atapatiwa matibabu mapema.